KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, October 14, 2016

SIMBA YAZIDI KUCHANUA LIGI KUU, YANGA YAIUA MTIBWA, JAHAZI LA AZAM LAZIDI KUZAMA


SIMBA imezidi kujikita kileleni mwa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu baada ya kuibanjua Mbeya City mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Mabao yaliyoiwezesha Simba kutoka uwanjani na pointi zote tatu, yalipachikwa wavuni na washambuliaji Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya, kipindi cha kwanza.

Kutokana na ushindi huo, Simba sasa inazo poinri 20 baada ya kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Stand United yenye pointi 17.

Ajib aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya ya sita kwa mpira wa adhabu uliotinga moja kwa moja wavuni, kufuatia Kichuya kuchezewa rfau ndani ya eneo la hatari.

Kichuya aliongeza bao la pili dakika ya 37 baada ya kuambaa na mpira pembeni ya uwanja na kufumua shuti lililotinga moja kwa moja wavuni.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga walizinduka baada ya kuicharaza Mtibwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Walioiwezesha Yanga kuwatoa kimasomaso mashabiki wao ni Mzambia, Obrey Chirwa, likiwa bao lake la kwanza tangu ligi ilipoanza, Simon Msuva na Donald Ngoma. Bao la Mtibwa lilifungwa na Haruna Chanongo.

Vigogo wengine wa ligi hiyo, Azam waliendelea kuwakosesha raha mashabiki wao baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Bao pekee na la ushindi la Stand United, ambayo wiki iliyopita iliifunga Yanga idadi hiyo ya bao kwenye uwanja huo, lilifungwa na Adam Salamba dakika ya 52.

No comments:

Post a Comment