KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 17, 2016

SIMBA YAZIDI KUCHANJA MBUGA, YAIBANJUA KAGERA SUGAR 2-0


SIMBA juzi iliendelea kujidhatiti kileleni mwa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Simba ilipata mabao hayo mawili, moja katika kila kipindi, wafungaji wakiwa Muzamil Yassin na Shiza Kichuya.

Kutokana na ushindi huo, Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa, ikifuatiwa na Stand United yenye pointi 20 baada ya kucheza mechi 10.

Iliwachukua Simba dakika 43 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Muzamil, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa kona maridhawa kutoka kwa Kichuya.

Kichuya aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 75 baada ya kuukwamisha mpira wavuni kwa njia ya penalti, iliyotokana na beki Juma Ramadhani wa Kagera Sugar kumwangusa Mo Ibrahim ndani ya eneo la hatari.

Katika mechi hiyo, wanasoka wa kulipwa wa Simba, Frederick Blagnon na Laudit Mavugo walishindwa kuonyesha uwezo wao, hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa mashabiki.

No comments:

Post a Comment