KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 16, 2014

YANGA YAMKARIBISHA KOCHA MPYA KWA USHINDI


Young Africans imemkaribish vizuri kocha mkuu mpya Hans Van Der Plyum leo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Altay SK iliyopo Ligi Daraja la pili nchini Uturuki katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika leo mchana katika viwanja vya Sueno eneo la Side Manavgat.
Kocha Hans ambaye aliwasili jana jioni na kuongea na wachezaji kwa pamoja kabla ya chakula cha usiku alisisitiza nidhamu, upendo na kujituma miongoni mwa wachezaji na benchi la ufundi kitu ambacho mpaka sasa amefurahishwa na ushirikiano anaopewa na wachezaji na viongozi kwa ujumla.
Ikiwa mechi yake ya kwanza kama kocha mkuu wa Young Africans Hans aliweza kukaka kwenye benchi pamoja na makocha Charles Mkwasa, Juma Pondamali, Hafidh Saleh na daktari wa timu Dr. Suphian Juma ambapo kwa pamoja kikosi kimeweza kuendeleza ushindi wa pili mfululizo.
Mechi ilianza kwa kasi kwa timu zote kusaka mabao ya mapema, lakini umakini wa walinzi wa timu zote mbili ilikuwa kikwazo kwa washmbuliaji wa timu zote kuweza kupata mabao kwani mipira yao mingi iliishia kuchezwa na walinzi na walinda milnago wa timu zote.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Altay SK 0 - 0 Young Africans.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 46 ya mchezo, mshambuliaji Didier Kavumbagu aliipatia Young Africans bao la kwanza baada ya kuitumia vizuri pasi ya kiungo Haruna Niyonzima na kuwatoka walinzi wa Altay na kumchambua golikipa wao na kuhasabu bao la kwanza kwa watoto wa jangwani.
Mara baada ya bao hilo, Altay walicharuka na kufanya mashambulizi ya nguvu ya kusaka bao la kusawazisha lakini mlinda mlango Ally Mustafa "Barthez" alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira miwili ya wazi iliyokuwa inaelekea wavuni na kuwa kona ambazo hazikuzaa matunda.
Dakika ya 57 ya mchezo mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi aliipatia Young Africans bao la pili na la ushindi baada ya kupokea pasi safi ya kiungo Haruna Niyonzima kabla ya mganda huyo kuukwamisha mpira wavuni na kuhesabu bao la pili.
Frank Domayo alikosa nafasi mbili za wazi za kufunga baada ya mashuti aliyopiga kupaa sentimite chache juu ya lango la Altay huku Hamsi Kiiza akikosa bao la wazi bada ya mpira alioupiga kugonga mwamba na kurudi uwanjani.
Hamis Kiiza alikosa penati dakika ya 83 ya mchezo baada ya mchomo wake kupanguliwa na mlinda mlango wa Altay SK kabla ya Kiiza tena kuuwahi kuumalizia na kutoka juu ya lango la Altay SK.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Altay SK 0 - 2 Young Africans
Kocha mkuu mpya wa Young Africans mholanzi Hans Van Der Plyum amesema timu yake imecheza vizuri na hasa kipindi cha pili, kwani kipindi cha kwanza wapinzani waliwaabana sana na kushindwa kupata bao lakini kipindi cha pili washambuliaji wake walitumia vizuri nafasi walizozipata na ndio maana timu ikapata ushindi.
"Huu ni mwanzo mzuri tupo hapa Uturuki kwa ajili ya kambi ya mafunzo, wachezaji wamecheza vizuri kwa kipindi hiki kilichobakia kabla ya kurejea Tanzania tutaendelea kuwaandaa vijana wake katika uwezo mzuri na tayari kwa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa" alisema Hans
Mara baada ya mechi ya leo timu itaendelea na mazoezi kesho asubuhi kuendelea kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya kimataifa.
Young Africans: 1.Ally Mustafa "Barthez", 2.Juma Abdul, 3.Oscar Joshua/David Luhende, 4.Mbuyu Twite, 5.Kelvin Yondani, 6.Frank Domayo, 7.Haruna Niyonzima, 8.Hassan Dilunga/Nizar Khalfani, 9.Didier Kavumbagu/Hamis Kiiza, 10.Emmanuel Okwi, 11.Mrisho Ngasa/Saimon Msuva

No comments:

Post a Comment