KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 16, 2014

RAMSEY: NIMEPITIA VIPINDI VIGUMU KATIKA MAISHA YANGU


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Ramsey Nouah amesema, amepitia vipindi mbalimbali vigumu katika maisha yake kabla ya kuibuka kuwa mcheza filamu mahiri nchini humo.
Ramsey, mmoja wa wacheza filamu wanaolipwa pesa nyingi nchini Nigeria, alisema hayo hivi karibuni alipohojiwa na gazeti la The Sun News la nchi hiyo.
Mcheza filamu huyo mwenye mvuto na ambaye ni mahiri kwa kucheza filamu za mapenzi, amesema kuna wakati alikaa bila kula kwa siku tatu hadi nne ikiwa ni pamoja na kuishi mitaani.
"Kuna wakati, wakati ule wa matatizo, hatukuwa na kitu, tuliishi kwa matatizo. Tulikuwa tukisaidiwa na watu. Kuna wakati tulishinda njaa kwa siku tatu hadi nne,"amesema mcheza filamu huyo mwenye mke na watoto wawili.
"Unashinda na njaa, tumbo lako halina kitu, lakini huna pa kwenda. Kuna wakati niliishi mitaani na kwenye maduka. Kuna wakati nilikuwa nalala chini ya daraja," aliongeza mcheza filamu huyo.
Ramsey amesema bahati nzuri ni kwamba hakuna kumbukumbu za maisha hayo ya dhiki aliyopitia, lakini huwa anayakumbuka vyema kila anapokumbuka alikotoka.
Mcheza filamu huyo mwenye mvuto amesema anashukuru kwa kupitia maisha hayo, ambayo kuna wakati yalimfanya amchukie kila mtu aliyekuwa karibu naye.
"Kiukweli, nilizoea kujiuliza kwa nini Mungu ananifanyia hivi? Lakini nafikiri Mungu alielewa kwamba, nilihitajika kuishi hivyo kwa ajili ya maisha yangu ya baadaye,"amesema Ramsey.
Mcheza filamu huyo amesema, watu wamekuwa wakiyatafsiri vibaya maisha yake kwa kumuona anaringa, lakini ukweli ni kwamba ni mtu wa kawaida na asiyependa kujikweza.
"Mara nyingi watu wengi wamekuwa wakinishutumu, lakini nikiwa mwigizaji, napaswa kukabiliana na mambo haya. Na ni rahisi kwa watu kunisema kwa sababu hakuna aliyevaa viatu vyangu.
"Wanigeria ni wepesi wa kuhukumu kwa sababu ni wazuri katika kusema maneno kabla ya kufikiri. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba sisi ni binadamu wa kawaida kama walivyo wengine. Mimi si Yesu na sipo hapa kuiokoa dunia,"amesema Ramsey.
  Amesema kuwa kwake muigizaji hakuna maana kwamba, amekuwa akipata kila anachokihitaji ama kuwa na maisha mazuri. Amesema watoto wake wamekuwa wakiugua na kupelekwa hospitali kama watoto wengine.
Licha ya ukimya wa muda mrefu, Ramsey amesema bado anaendelea kucheza filamu na anamuomba Mungu fani hiyo ipige hatua kubwa kimaendeleo nchini Nigeria kuliko ilivyo hivi sasa.
Ramsey amesema licha ya mafanikio waliyofikia, wacheza filamu wa Nigeria hawana mafanikio makubwa na hilo limekuwa likiwaathiri na kuwafanya wasiwe na uhakika wa maisha yao ya baadaye.
"Kwa mfano, baadhi ya wacheza filamu wakongwe wamekufa wakiwa masikini na mazishi yao yalifanyika kwa kuchangiwa na watu kwa lengo la kuwapa heshima,"amesema Ramsey.
Ili kuifanya fani hiyo ipige hatua kubwa zaidi kimaendeleo nchini Nigeria, Ramsey amesema wanapaswa kutengeneza filamu za kiwango cha juu,ambazo zitadumu na kuwa na mvuto kwa miaka mingi.
"Lazima kuwepo na mabadiliko. Bila fani yetu kukua, hatuwezi kuwa na maisha mazuri.  Mashabiki wamechoka kuona kitu kilekile. Hii ndiyo sababu iliyonifanya niwe kimya kwa muda.
"Naipenda kazi ya uigizaji. Napenda kufanyakazi, ambayo italeta mafanikio katika fani. Napenda kucheza filamu, ambayo unaweza kuitazama kwa miaka mitano au 20 na kuifurahia. Nataka kuacha alama na kumbukumbu si kuuza sura,"amesema.

No comments:

Post a Comment