KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 30, 2014

TIKETI ZA ELEKTRONIKI BADO TATIZO-MWESIGWA



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limekiri kutokea kwa baadhi ya matatizo kwenye viwanja, ambavyo vimeanza kutumia mfumo wa uuzaji wa tiketi kwa njia ya elektroniki.

Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema mjini Dar es Salaam, wiki hii kuwa, matatizo hayo yametokana na ugeni wa teknolojia hiyo kwa mashabiki.

"Unajua kitu kinapoanza kwa mara ya kwanza, hasa inapotumika teknolojia mpya, lazima yajitokeze matatizo. Na hivyo ndivyo ilivyotokea katika baadhi ya viwanja na tumeshaanza kuyafanyia kazi matatizo hayo ili kuiboresha huduma hiyo,"alisema Mwesigwa.

Aliongeza kuwa, hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya mapato iliyopatikana katika viwanja vilivyoanza kuuza tiketi kwa kutumia mfumo huo, lakini aliahidi watazipata baada ya siku chache zijazo.

Mwesigwa alisema uuzaji wa tiketi za elektroniki umeshindwa kutumika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kutokana na idadi kubwa ya mashabiki wanaofika uwanjani, hasa katika mechi za Simba na Yanga.

Alisema waliamua utaratibu huo uanze kwanza kwenye viwanja vya mikoani ili kuona faida na hasara zake kabla ya kuuhusisha Uwanja wa Taifa, ambao unachukua idadi kubwa ya mashabiki.

Katibu Mkuu huyo wa TFF alisema ana hakika baada ya siku chache zijazo, tiketi za elektroniki zitaanza kutumika kwenye uwanja huo baada ya kufanyika tathmini kwenye viwanja vingine.

Alisema utaratibu huo ni mzuri kwa vile unasaidia kupunguza msongamano wa watu wakati wa kuingia uwanjani na vilevile unaepusha wizi wa tiketi na mapato ya milangoni.

Mwesigwa alisema TFF inaamini kuwa, uuzaji wa tiketi kwa njia hiyo utazisaidia klabu kupata mapato mengi, tofauti na ilivyo sasa, ambapo baadhi ya wajanja wachache wamekuwa wakitengeneza na kuuza tiketi feki.

Aliongeza kuwa TFF imeshaanza kutoa elimu kwa mashabiki kuhusu utaratibu wa kununua tiketi hizo ili kuepusha usumbufu kwa wale, ambao hawaujui. Alisema wamekuwa wakitoa elimu hiyo kupitia matangazo ya kwenye redio na televisheni.

No comments:

Post a Comment