KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 23, 2014

ROSE MUHANDO: SIJAWAHI KUTAFUNA PESA ZA PROMOTA NA KUINGIA MITINI


MWIMBAJI nyota wa nyimbo za muziki wa Injili nchini, Rose Muhando amesema kamwe hajawahi kutafuna pesa za mapromota na kukwepa kufanya maonyesho.

Rose amesema kwa kipindi cha miezi sita iliyopita, ameshindwa kushiriki kwenye matamasha mbalimbali ya muziki huo kutokana na binti yake kuwa mgonjwa.

Mwimbaji huyo anayeongoza kwa mauzo ya nyimbo za muziki wa Injili, ametoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya mapromota kwamba, amekuwa akilipwa pesa na kukwepa kushiriki kwenye maonyesho yao.

Malalamiko mengine yaliyokuwa yakimuhusisha msanii huyo ni baadhi ya mapromota kuonekana waongo kwa kutumia jina la Rose wanapoandaa matamasha kwa lengo la kuvuta idadi kubwa ya mashabiki.

Hii ilifanya baadhi ya watu kukwazika, baadhi ya mapromota kuonekana waongo na kuonekana kama walitaka kujikusanyia kiingilio au kupata idadi kubwa ya watu kwa kutumia tu jina la Rose lakini hakuna kitu.

"Kwa kipindi cha miezi sita sikuweza kwenda kwenye tamasha lolote lile kwa sababu binti yangu ni mgonjwa mpaka sasa,"amesema Rose alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM juzi.

"Sina tabia hiyo na wala siwezi kufanya hicho kitu. Kila ambaye amenilipa pesa yake, nimeanza kuzirudisha tangu muda mrefu uliopita. Nawaomba wawe na amani na mimi niwe na amani," amesema mwanamama huyo mwenye watoto wanne.

"Mimi ni mama na ni binadamu kama wengine na ninapata matatizo ndio maana siwezi kumuacha binti yangu hoi kitandani wakati ananitegemea mama yake mzazi.Hata roho mtakatifu ataniona ni mwanamke mjinga kuliko wote, ni heri niwe sina kitu manake kama sina, Bwana Yesu atanipa tu, atanipa mara mia zaidi," amesisitiza mwimbaji huyo.

Katika hatua nyingine, Rose amesema tangu alipoingia mkataba na Kampuni ya Sony ya Afrika Kusini, amefanikiwa kurekodi wimbo mmoja unaokwenda kwa jina la Yesu kung'uta.

Rose amesema alirekodi video ya wimbo huo, ambao pia unajulikana kwa jina la Wololo, nchini Afrika Kusini. Alirekodi wimbo huo Julai mwaka jana.

Mwimbaji huyo machachari, aliingia mkataba na Sony miaka miwili iliyopita kwa lengo la kuongeza mapato na kujitangaza kimataifa.

Kwa mujibu wa Rose, wimbo huo ulichelewa kutoka kwa sababu ilibidi amalizie kurekodi video kwa vile isingekuwa rahisi kutoa audio kabla ya video.

"Hii ni kwa mujibu wa taratibu za ofisi, huwezi kutoa audio kabla ya video,"amesema Rose.
Mwanadada huyo amesema, tangu alipoanza kufanyakazi na Sony, ameona tofauti kubwa, ikiwa ni pamoja na kutoachiwa kufanya vitu vyote peke yake.

"Vitu vingi sifanyi mwenyewe, ninachofanya ni kuandaa nyimbo zangu ila vingine sijui nitavaa nguo gani, nitapanda gari au ndege gani, kila kitu ni wao," amesema.

Rose amesema tangu alipoanza kufanyakazi na Sony, wapo wanaoufurahia uamuzi wake huo, lakini wengine wamechukia, lakini kamwe hawezi kuwajali.

"Mungu akisema imeandikwa, nitafanya kama ilivyoandikwa. Mungu akiniambia fanya, ninafanya, haijalishi kuna mtu anataka au kuna mtu hataki," amesema Rose.

No comments:

Post a Comment