KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, January 10, 2014

SIMBA YATINGA FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI, YALIPA KISASI KWA URA




SIMBA SC wamefuzu kuingia Fainali ya Kombe la Mapinduzi, baada ya usiku huu kuilaza mabao 2-0 URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.


Shujaa wa Simba SC leo alikuwa ni kiungo mwenye kipaji, Amri Ramadhani Kiemba aliyesababisha bao la kwanza na kufunga mwenyewe la pili.

URA ilipata pigo mapema dakika ya 32 baada ya mshambuliaji wake hatari, Owen Kasuule kutolewa nje kwa nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea rafu winga msumbufu wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’. 



Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na kipindi cha pili ndipo Simba SC inayofundishwa na Mcroatia, Zdravko Logarusic ilipofungua makucha yake.

Kona maridadi ya Kiemba ilimkuta beki Donald Mosoti, aliyemsetia beki pacha wake wa kati, Joseph Owino akafunga bao la kwanza dakika ya 49.

Wakati URA wanahaha kusaka bao la kusawazisha, Simba SC walifanya shambulizi zuri na krosi maridadi ya Haroun Chanongo ikaunganishwa nyavuni na Amri Kiemba dakika ya 52 kuipatia Simba SC bao la pili.

Bao hilo liliinyong’onyesha kabisa URA, ingawa iliendelea kupambana kupata japo bao la kufutia machozi.

Kwa ujumla, URA iliathiriwa mno na kutolewa na mshambuliaji wake hatari, Owen Kasuule, kwani ndiye tegemeo lake la mabao kwa pamoja na Feni Ali.

Baada ya mechi, Kiemba alipewa king’amuzi cha Azam TV kwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

Simba SC sasa itapambana na KCC ya Uganda pia katika Fainali Jumatatu Saa 10:00 Uwanja wa Amaan.

Ikumbukwe Simba na KCC zote zimetokea Kundi B na katika mechi baina yao, zilitoka sare ya bila kufungana.

Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’/William Lucian 'Gallas', Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Amri Kiemba/Said Ndemla, Ramadhani Singano ‘Messi’, Amisi Tambwe/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Awadh Juma/Uhuru Suleiman.

URA; Mugabi Yassin, Samuel Ssenkoom, Alan Munamba/James Kasibante, Mussa Doca, Jonathan Mugabi, Oscar Agaba, Augustine Nsumba, Owen Kasuule, Erisa Sekisambu/Ngama Emmanuel, Feni Ali/Milos Ilic na Hashimu Sempalia.   IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment