KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 23, 2014

KUMEKUCHA LIGI KUU BARA


MZUNGUKO wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, unatarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokutwa katika mechi tano zitakazochezwa kwenye viwanja vitano tofauti.

Katika mechi hizo, mabingwa watetezi Yanga watamenyana na Ashanti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu. Katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1.

Yanga iliweka kambi Uturuki kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko huo na inatarajiwa kurejea nchini kesho. Ashanti ilitumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi kujiandaa na mzunguko huo.

Katika mechi zingine zitakazochezwa keshokutwa, Azam wataikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, ulioko Mbagala, Dar es Salaam, Coastal Union itakipiga na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Mkwakwa, Tanga, Kagera Sugar itavaana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wakati Prisons itamenyana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Awali, mechi kati ya Prisons na Ruvu ilipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Sokoine wa Mbeya, lakini imehamishiwa Samora kutokana na eneo la kuchezea mpira kutokuwa  na nyasi.

Uwanja wa Sokoine ni miongoni mwa viwanja sita vilivyofungiwa na Bodi ya Ligi Kuu kutumika katika ligi kutokana na kuwa na kasoro mbalimbali.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho wakati timu kongwe ya Simba itakapomenyana na Rhino Rangers ya Tabora wakati JKT Ruvu itamenyana na ndugu zao wa Mgambo JKT kwenye uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi hizo yamekamilika.

Wambura alisema pia kuwa, matumizi ya tiketi za elektroniki yanaanza katika mzunguko huu kwa vile tayari viwanja vinane vimeshafungwa vifaa vya tiketi hizo.

Ofisa huyo wa TFF alitoa onyo kwa mashabiki kuepuka kununua tiketi kupitia mikononi mwa watu binafsi kwa vile tiketi za elektroniki haziuzwi viwanjani.

No comments:

Post a Comment