KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 23, 2014

MKUTANO MKUU SIMBA MACHI 23, MZEE KINESI AVULIWA UMAKAMU MWENYEKITI, KAMWAGA KATIBU MKUU MPYA, ASHA MUHAJI AWA OFISA HABARI



NA AMINA ATHUMANI

MWENYEKITI wa Klabu ya Simba Ismail Rage amesema ataitisha mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo utakaofanyika Machi 23 mwaka huu.

Mkutano huo utakuwa na ajenda moja tu ya marekebisho ya katika ya klabu hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rage alisema atauendesha mkutano huo kwa ajenda moja kwani tayari mkutano wa kikatiba wa klabu hiyo wa kila mwaka ulishafanyika Agosti mwaka jana.

"Mkutano huu utakuwa na ajenda  moja tu na yoyote atakayeleta mambo ambayo hayamo ndani ya ajenda hiyo nitamkalisha chini ama kumtoa nje  ya ukumbi, mimi ndiye nitakayeendesha mkutano huo kama vile Spika wa bunge anavyolimiliki bunge lake na sitaruhusu mtu akurupuke kama vile anatoka chooni,"alisema Rage.

Rage alisema amepata barua mbili kutoka Shirikisho la soka Tanzania (TFF) moja  ikitumwa Desemba 2 na nyingine Desemba 30 ambazo zimetaka vyama kufanya marekebisho ya katiba zao huku nyingine ikimtaka aitishe uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya makamu Mwenyekiti.

Rage alisema katika marekebisho ya Katiba amegundua kuna upungufu katika katiba ya Simba  ambayo haina kamati ya maadili na katika mkutano huo wataiweka kamati hiyo baada ya marekebisho hayo.

Alisema pia ndani ya Katiba ya Simba amegundua vipo vipengele vya Simba ambavyo vimepitwa na wakati hivyo vinahitaji kuondolewa.

Alisema pia kuanzia sasa klabu ya Simba haina makamu Mwenyekiti nafasi ambayo ilikuwa ikiongozwa na Joseph Itang'are 'kinesi' na kwamba ataiomba TFF kama itawezekana kuufanya uchaguzi mkuu mapema kwa kuwa mchakato wa kufanya uchaguzi mdogo utatatakiwa kufanyika ndani ya siku 90.

"Kwa maana hiyo ukifanya mchakato ndani ya siku 90 na sisi kikatiba tunatakiwa kufanya uchaguzi Juni, huyo atakayechaguliwa atakaa madarakani kwa mwezi mmoja tu itakuwa haina maana yoyote,"alisema Rage.

Alisema kwa maana hiyo nafasi hiyo ni bora ibaki wazi hadi hapo uchaguzi mkuu utakapofanyika kwani katiba ya Simba ipo wazi na atakapokuwa hayupo nchini atamteuwa mtu yoyote ndani ya Sekretarieti ya Simba kukaimu nafasi yake.

Wakati huo huo, Rage amemteuwa Ezekiel Kamwaka kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo akisaidiana na Stanley Philipo na nafasi ya Ofisa Habari akimpa Asha Muhaji.

No comments:

Post a Comment