KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 16, 2014

CHUJI AKALIA KUTI KAVU YANGA


 
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umekiri kupokea barua ya kuomba msamaha kutoka kwa kiungo wa timu hiyo, Athuman Idd 'Chuji', ambaye amesimamishwa kwa muda usiojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema Chuji aliwasilisha barua ya kuomba radhi kwa uongozi wiki iliyopita.
Sanga alisema kamati ya utendaji ya klabu hiyo inatarajiwa kukutana hivi karibuni kujadili barua hiyo ya Chuji kabla ya kutoa uamuzi.
"Ukweli ni kwamba hatutaki kumkomoa mchezaji huyo, tumechukua uamuzi wa kumsimamisha kutokana na sababu mbalimbali, hivyo tutakutana kuijadili barua yake na kutoa uamuzi siku chache zijazo,"alisema Sanga.
Kamati ya Utendaji ya Yanga, ilimsimamisha Chuji kwa kosa la kushindwa kuripoti mazoezini wakati timu hiyo ilipokuwa ikijiandaa kwa safari ya Uturuki.
Chuji pia anadaiwa, kucheza chini ya kiwango wakati Yanga ilipomenyana na Simba katika mechi ya 'Nani Mkali Jembe' na kuchapwa mabao 3-1 na kuonyesha ujeuri baada ya kutolewa kipindi cha pili.
Mbali na kumsimamisha Chuji, kamati ya utendaji ya Yanga pia iliamua kulifumua benchi lote la ufundi kwa kuwaondoa kocha Ernie Brandts, msaidizi wake, Fred Felix Minziro na kocha wa makipa Razack Siwa.
Nafasi ya Brandts imechukuliwa na kocha mpya, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm kutoka Uholanzi, akisaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali.
Wakati huo huo, Yanga imewataka wanachama wake kulipia kadi zao za uanachama
ili waweze kushiriki katika mkutano mkuu uliopangwa fanyika Januari 19 mwaka huu
ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam.
Ajenda za mkutano huo zitatolewa kwenye kikao cha viongozi wa matawi ya klabu hiyo, kitakachofanyika kesho makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment