KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 30, 2014

AZAM YAISHUSHA YANGA KILELENI, MBEYA CITY YABANWA


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga jana walishindwa kutamba mbele ya Coastal Union baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Sare hiyo imeifanya Yanga ienguliwe kutoka kileleni mwa ligi hiyo baada ya Azam kuishinda Rhino Rangers bao 1-0 na kuwa mbele ya mabingwa hao kwa tofauti ya pointi moja.

Azam inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 15, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 32 na Mbeya City yenye pointi 31.

Yanga ilizianza dakika tatu za kwanza kufanya mashambulizi kwenye lango la Coastal Union, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini katika kulenga lango la wapinzani wao.
Coastal Union nayo ililishambulia mfululizo lango la Yanga dakika 30 za kwanza, na kama si uhodari wa kipa Deogratius Bonaventura 'Dida' kuzuia mashuti ya Haruna Moshi, Yaya Lutimba na Kenneth Masumbuko, huenda hadithi ingekuwa nyingine. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji katika kipindi cha pili, lakini hayakuweza kuzisaidia kubadili sura ya mchezo.

Katika hatua nyingine, tiketi za elektroniki jana zilishindwa kufungua milango ya kwenye Uwanja wa Mkwakwani na kusababisha tafrani kubwa.

Kwa mujibu wa utaratibu mpya, mashabiki huzitumia tiketi hizo kufungua milango, lakini ilishindikana na kusababisha kutokea kwa vurugu.

Kutokana na kadhia hiyo, ilibidi utaratibu wa kawaida utumike kwa mashabiki kwenda na tiketi zao mlangoni na kuchanwa na walinzi wa milangoni.

YANGA: Degratius Bonaventura 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Cannavaro, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na David Luhende/Jerry Tegete.

COASTAL UNION: Shabani Kado, Shabani Hamisi, Abdi Banda, Mbwana Hamis, Juma Nyosso, Jerry Santo, Danny Lyanga, Crispine Odula, Yayo Lutimba, Haruna Moshi 'Boban' na Kenneth Masumbuko.

Wakati huo huo, Azam jana iliishusha Yanga kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuichapa Rhino Rangers bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi ulioko Mbagala, Dar es Salaam.

Bao pekee na la ushindi la Azam lilipachikwa wavuni na mshambuliaji Kipre Tchetche kipindi cha kwanza na kumfanya alingane na Hamisi Tambwe wa Simba kwa ufungaji mabao, wote wakiwa wamefunga mabao 10 kila mmoja.

Mbeya City  ilishindwa kutamba mbele ya Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya bao 1-1 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizo mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment