KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 30, 2014

OWINO AIVIMBIA SIMBA


HATMA ya beki Joseph Owino katika klabu ya Simba, imeendelea kuwa shakani baada ya kugoma kwenda kufanya mazoezi na kikosi cha pili cha timu hiyo.

Owino alitakiwa kuanza mazoezi na kikosi hicho jana asubuhi kwenye uwanja wa Kinesi ulioko Urafiki, Dar es Salaam.

Hata hivyo, beki huyo kutoka Uganda, hakuweza kuhudhuria mazoezi hayo na hakutoa taarifa yoyote kwa Kocha wa timu hiyo, Selemani Matola.

Alipoulizwa jana iwapo Owino alihudhuria mazoezi ya kikosi cha pili, Matola alisema:
"Sijamwona Owino na sifahamu habari zake, waulize viongozi."

Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic aliamua kumshusha beki huyo kwenye kikosi cha pili baada ya kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu wakati wa mazoezi yaliyofanyika wiki iliyopita.

Logarusic aliwaeleza viongozi wa klabu hiyo kwamba, amechoshwa na tabia za mchezaji huyo kwa madai kuwa, hana nidhamu na amekuwa akijisikia kwa kujiona yuko juu ya kocha na wachezaji wenzake.

Alipoulizwa jana kuhusu sakata la mchezaji huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Asha Muhaji alisema kwa sasa lipo mikononi mwa benchi la ufundi.

"Suala la Owino kwa sasa lipo mikononi mwa benchi la ufundi, halipo kwa uongozi.
Tunachofahamu kwa sasa ni kwamba kocha ameamua kumshusha kikosi cha pili na ni lazima atekeleze adhabu hiyo,"alisema Asha.

Kwa mujibu wa Asha, Owino alipaswa kuanza mazoezi na kikosi cha pili jana chini ya Kocha Msaidizi, Matola, ambaye pia amepewa jukumu la kukinoa kikosi hicho.

Alisema Kocha Logarusic ameamua kumshusha Owino kikosi cha pili kutokana na kushindwa kufikia vigezo anavyovihitaji na huo ni uamuzi wa kawaida kwa kocha yoyote.

"Jambo la msingi ni kwa Owino kutii adhabu hiyo. Anaweza kufanya mazoezi na kikosi cha pili kwa siku tatu au wiki moja, na iwapo ataonekana amejirekebisha, atarudishwa kikosi cha kwanza," alisisitiza Asha.

No comments:

Post a Comment