KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 30, 2014

NANI KASEMA BONGO FLEVA HAILIPI?


MWAKA 2014 umeanza kwa wasanii kadhaa wa muziki wa kizazi kipya nchini, maarufu kwa jina la bongo fleva kuonyesha mali wanazozimiliki au nyumba walizojenga na kununua.

Lengo la wasanii hao kuonyesha mali zao hizo ni kuithibitishia jamii kwamba, muziki wa kizazi kipya unalipa, tofauti na mawazo yaliyotawala vichwani mwa watu wengi.

Alianza Naseeb Abdul 'Diamond', ambaye kupitia mitandao mbalimbali, alionyesha gari lake aina ya Land Cruiser lenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 60. Ni bonge la 'mkoko', si mchezo.

Akafuata Judith Wambura, maarufu kwa jina la Lady Jaydee. Naye pia alionyesha gari lake jipya aina ya Jaguar, lenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 20.

Hivi karibuni, mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS), Emmanuel Msuya, ambaye alizawadiwa kitita cha sh. milioni 50, naye ameonyesha jinsi alivyozitumia pesa hizo.


Kabla ya kubahatika kupata kitita hicho cha pesa, Msuya hakuwahi kushika au kumiliki zaidi ya sh. 500,000. Aliwahi kupata kiasi hicho cha pesa mara moja, alipolipwa posho ya miezi mitatu iliyotokana na kuifundisha na kuisimamia kwaya ya KKKT kucheza ili ikafanye onyesho.

Mambo matatu makubwa, yaliyofanywa na Msuya baada ya kupata kitita hicho cha BSS ni kununua nyumba yenye thamani ya sh. milioni 17 iliyoko nyumbani kwao Musoma Mjini.

Msuya pia amenunua gari lenye thamani ya sh. milioni tisa na pia amejenga studio ya kurekodi muziki, ambayo imemgharimu sh. milioni 12 na tayari amepata nyumba ya kufanyia biashara ya vifaa vya shule katika moja ya mitaa ya Musoma Mjini.

Msanii mwingine aliyeamua kuweka mali zake hadharani ni Jux, ambaye hivi karibuni, video yake ya Uzuri wako, aliyeirekodi China, ilifungiwa kuonyeshwa kwenye luninga.



Jux aliamua kuonyesha gari lake jipya aina ya Nissan Fuga, lakini hakuwa tayari kutaja thamani yake. Lakini kwa kawaida, magari ya aina hii yanauzwa kati ya dola 2,000 na dola 4,000, ambazo ni zaidi ya sh. milioni sita za Kitanzania. Hapo bado gharama za kulisafirisha, kulipa ushuru na mambo mengine muhimu.

Kwa mujibu wa Jux, amenunua gari hilo kwa pesa, ambazo zimetokana na biashara anazozifanya. Hakuziweka wazi biashara hizo.

Naye David Geez, maarufu kwa jina la Young D, ameonyesha picha za nyumba aliyonunua maeneo ya Kimara Suka, Dar es Salaam.


Nyumba hiyo iliwahi kutumika ikiwa haijamaliziwa. Msanii huyo amesema ataifanyia ukarabati mkubwa ili iweze kufikia kiwango anachokitaka yeye kabla ya kuhamia na kuishi huko.

Msanii mwingine aliyeamua kuonyesha mali zake ni Barnaba Elias. Huyu alionyesha nyumba yake anayoijenga maeneo ya Tabata na gari lake jipya aina ya Toyota Mark X.


Barnaba ni msanii mwenye kipaji cha aina yake katika kuimba na kutunga nyimbo zenye mvuto. Amekuwa akialikwa kufanya maonyesho katika sehemu mbalimbali, ndani na nje ya nchi.

Msanii huyo wa kundi la THT pia amekuwa akipata dili kutoka kwenye mashirika, taasisi na kufanya nazo kazi mbalimbali, ikiwemo kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsui na benki ya Barclays.

Hii yote imedhihirisha kwamba, wasanii wa bongo fleva wanaweza kufaidika iwapo watakuwa na mpangilio mzuri wa matumizi kutokana na fedha wanazolipwa katika maonyesho na mauzo ya nyimbo na albamu zao.

Wapo baadhi ya wasanii waliobahatika kupata pesa nyingi miaka ya nyuma kutokana na muziki huo, lakini hawakuweza kufika popote kwa sababu ya kutokuwa na nidhamu katika matumizi ya pesa zao. Waliendekeza zaidi starehe.

No comments:

Post a Comment