KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, January 29, 2014

KUMEKUCHA SIKINDE, YAIPUA VIBAO VIPYA SABA

Waimbaji wa bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park, Hassan Bitchuka na Abdalla Hemba wakiwajibika jukwaani katika moja ya maonyesho yao.

BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde', imeanza kurekodi vibao vyake vipya saba, ikiwa ni maandalizi ya kuitambulisha albamu mpya.

Katibu wa bendi hiyo, Hamisi Milambo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kwanza kuanzia, wamesharekodi vibao vinne kati ya saba.

Milambo alisema wamerekodi vibao hivyo kwenye studio za Sound Crafters, zilizoko Temeke, Dar es Salaam.

Alivitaja vibao hivyo kuwa ni Tabasamu kilichotungwa na mwimbaji, Hassan Bitchuka, Mkwezi kilichotungwa na Abdalla Hemba, Nitalipa deni kilichotungwa na mpiga solo, Ramadhani Mapesa na Jinamizi la Talaka kilichotungwa na wanamuziki wote.

Milambo alisema vibao vingine vitatu, vinatarajiwa kurekodiwa mwishoni mwa wiki hii kwenye studio hizo. Alivitaja vibao hivyo kuwa ni Dole gumba, kilichotungwa na Bitchuka, Nundule kilichotungwa na Mapesa na Kibogoyo, kilichotungwa na wanamuziki wote.

Katibu huyo wa Sikinde alisema albamu mpya ya bendi hiyo itakuwa na vibao saba na itatambulishwa wakati wa tamasha la kusherehekea miaka 36 ya bendi hiyo.

"Tunachopenda kuwaeleza mashabiki wetu ni kwamba, Sikinde kwa sasa imekamilika katika kila idara. Kwa sasa tupo katika maandalizi ya kuzindua albamu yetu mpya na tayari tumesharekodi nyimbo mpya nne kati ya saba,"alisema.

Wakati huo huo, kwa mara ya kwanza, bendi ya Mlimani Park inatarajiwa kufanya onyesho kesho kwenye ukumbi wa Meeda ulioko Sinza, Dar es Salaam.

Milambo alisema jana kuwa, wameamua kufanya onyesho kwenye ukumbi huo kutokana na maombi mengi ya mashabiki.

Kwa mujibu wa Milambo, keshokutwa bendi hiyo itafanya onyesho kwenye ukumbi wa Pentagon, ulioko Kurasini wakati Jumapili itaendelea kuwapa maraha mashabiki wake kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment