KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

Wema alazwa Mwananyamala kwa saa mbili

MREMBO wa zamani wa Tanzania, Wema Sepetu juzi alilazwa kwa saa mbili kwenye Hospitali ya Rufani ya mkoa wa Mwananyamala kutokana na kuishiwa nguvu.
Wema alipelekwa kwenye hospitali hiyo baada ya kuanguka wakati wa mazishi ya msanii nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba yaliyofanyika juzi.
Mbali na Wema, wanawake wengine 11 walifikishwa kwenye hospitali hiyo juzi kutokana na kuishiwa nguvu na kujeruhiwa wakati wa mazishi hayo.
Katibu wa Afya wa Hospitali ya Rufani ya Mwananyamala, Edwin Bisakala alisema jana kuwa, wagonjwa wawili walihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Bisakala alisema wema alilazwa kwenye hospitali hiyo kwa saa mbili na baada ya kupatiwa matibabu, aliruhusiwa kurejea nyumbani.
“Tatizo la Wema lilikuwa kuishiwa nguvu kama ilivyokuwa kwa wenzake wengine, lakini pia walikuwepo waliojeruhiwa,”alisema.
Mamia ya watu juzi walipoteza fahamu baada ya kushuhudia jeneza la Kanumba lilipofikishwa kwenye viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam kwa ajili ya kuagwa.
Mwili wa mcheza filamu huyo ulizikwa juzi mchana kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo maelfu ya watu walijitokeza kumsindikiza katika safari yake ya mwisho.
Kanumba alifariki dunia Jumamosi iliyopita baada ya kutokea ugomvi kati yake na rafiki yake wa kike, Elizabeth Michael ‘Lulu’, nyumbani kwake, Sinza Vatican mjini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment