KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 4, 2012

Rage awaonyesha undava Waalgeria

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismael Aden Rage juzi aliamua kutumia pesa zake kuisafirisha timu hiyo kwa ndege kutoka katika mji wa Algiers kwenda katika mji mwingine jirani na Setif.
Uamuzi huo wa Rage ulitokana na uongozi wa ES Setif kutaka kuisafirisha timu hiyo kwa basi kutoka Algiers kwenda Setif jana, umbali unaokadiriwa kufika kilometa 200.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Rage alisema alifikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, lengo la wapinzani wao lilikuwa ni kuwachosha wachezaji wa Simba.
Kwa mujibu wa Rage, umbali kutoka katika mji huo mdogo kwenda Setif ni kilometa 100 na kwamba alitumia dola 1900 kwa ajili ya kulipia msafara wao wote kwa ndege.
Alisema mara baada ya kufika kwenye mji huo mdogo, walipanda basi kwenda Setif tayari kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya ES Setif inayotarajiwa kuchezwa kesho usiku.
Rage alisema uongozi wa ES Setif umeahidi kumrejeshea fedha hizo kabla ya pambano kati yao. Alisema alitoa fedha hizo kutoka mfukoni mwake.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema anamshukuru Mungu kwamba wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wana ari kubwa ya kushinda mechi hiyo.
Rage alisema juzi, kikosi hicho cha Simba kilifanya mazoezi kwenye uwanja wa kikosi cha zimamoto kilichopo katika mji wa Algiers. Mazoezi hayo yalifanyika chini ya Kocha Milovan Cirkovic.
Aliwashukuru vijana wa Kitanzania wanaosoma nchini Algeria wenye itikadi za Simba na Yanga kwa kuwaunga mkono na kusafiri nao kutoka Algiers hadi Setif kwa ajili ya kuwashangilia.
Alisema vijana hao wametoa msaada mkubwa katika kufanikisha kupatikana kwa chakula kwa ajili ya wachezaji baada ya kubaini kuwa, wanaweza kuhujumiwa na wapinzani wao kwa kupewa chakula kibovu.
‘Sisi kama viongozi tumeamua wachezaji wasile chakula cha wenyeji wetu, tumeamua timu iwe inajipikia chakula chake ili kukwepa kuhujumiwa na wapinzani wetu,”alisema.
Rage alisema wamekuwa wakipambana na mbinu mbalimbali za kuwakatisha tamaa zinazofanywa na wenyeji wao tangu walipowasili Algiers, ikiwa ni pamoja na kucheleweshwa uwanja wa ndege kwa saa kadhaa na mizigo yao kuzuiwa na watu wa Idara ya Uhamiaji.
ES Setif (Tai Mweusi) ilianzishwa katika mji wa El Kahla mwaka 1958, ambako inamiliki uwanja wake uitwao Ground Stade 8 Mai 1945, wenye uwezo wa kuchukua watu 30,000 kwa wakati mmoja wakiwa wamekaa.

No comments:

Post a Comment