KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 7, 2012

KIFO CHA KANUMBA NI PIGO KUBWA-WASANII

VICENT KIGOSI RAY

WILLIAM MTITU

SANDRA

STEVE NYERERE


MONALISA

CLOUD

IRENE UWOYA

WASANII mbalimbali wa fani ya filamu nchini wameelezea hisia zao kutokana na kifo cha msanii mwenzao, Steven Kanumba kilichotokea usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam.
Baadhi ya wasanii hao wamesema kifo cha Kanumba kimeacha pigo kubwa katika tasnia ya filamu nchini na kwamba si rahisi pengo lake kuzibika. Zifuatazo ni kauli zilizotolewa na baadhi ya wasanii.
VICENT KIGOSI ‘RAY’

Kanumba alikuwa mtu aliyependa kupambana ili kutimiza ndoto na tulianza kupendana tangu tukiwa hatuna pesa (wakipanda daladala) hadi tulipoachana na usafiri huo wa umma kwa kuanza kutumia magari binafsi.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha Kanumba, nilifika nyumbani kwake na kujitahidi kutaka kujua kilichomsibu rafiki yangu kwa kumshika na kumtikisa bila mafanikio.
Nilipofika nilianza kumuita, nikamshika mkono na kumtikisa tikisa, lakini hakuna nilichofanikiwa. Kanumba alikuwa amefariki dunia.
Mimi na Kanumba tulikuwa na mashindano. Yeye akifanya hiki, mimi nafanya kile, lakini hivyo ndivyo ilivyo maana hata tulipoanza na filamu ya Johari, tulikuwa watu wa kawaida sana.
Kimsingi Kanumba hakupenda tu aonekane yeye, lakini alitaka na wengine wafahamike na zaidi alijitahidi sana kuitangaza Tanzania duniani.
Ingekuwa vipi hata bendera ya nchi ingepepea nusu mlingoti kwa sababu ya Kanumba maana ameitangaza sana nchi yetu huko nje, kiasi kwamba hakuna wasikomjua-kaenda Uingereza, Nigeria, Kongo, Uganda, Marekani na sehemu nyingi tu akitangaza sanaa hii na jina la Tanzania.
Urafiki wetu ulifika mahali tukawa kama ndugu, lakini zaidi ulikuwa wa (urafiki) wa kimashindano zaidi mathalan, yeye alipomleta Ramsey Noah (nyota wa filamu wa Nigeria), mimi nilikuwa nafikiria kumleta nyota mmoja wa Ghana. Pia viwanja vyetu tumenunua jirani jirani huko Mbezi Mpiji na tulipanga kuanza kujenga pamoja.
STEVE NYERERE

Kanumba alikuwa tegemeo langu kubwa katika sanaa na ni yeye pamoja na Ray (Vincet Kigosi) walinipa wazo la kucheza filamu, nikaamua kuanza na Mr. President. Hata juzi, mimi na Ray tulikuwa naye pale Club Maisha, ambapo yeye alikuwa juu anakunywa bia zake na sisi tulikuwa chini na Twanga Pepeta ilikuwa inatumbuiza pale.
Kama asingekuwa Kanumba, mimi nisingekuwa na maisha niliyo nayo, hata gari nililonalo nisingelipata maana ni yeye na Ray ndio walionisaidia kufika hapa nilipo.
ISSA MUSSA 'CLOUD’

Naweza kumueleza Kanumba kwamba alikuwa msanii mbunifu, aliyependa kujituma na kila unakokwenda, ilikuwa lazima kumkuta. Hakuchagua sana maishani mwake, iwe kwenye 'fasheni shoo', muziki au kokote, lazima utaikuta sura yake. Hali hiyo inaonyesha alikuwa mtu wa aina gani.
Sisi wasanii wa filamu tumepata pigo, lakini sio letu pia la Watanzania na Waafrika kwa ujumla. Kwa upande wa wasanii, pigo hili linatukumbukusha wenzetu wa Bongo Fleva walivyompoteza Mtoto wa Dandu (James Ndandu). Sina zaidi ila tunapaswa kumuombea Kanumba maana safari yake ameimaliza na alichotuachia ndicho tunachopaswa kuiga.
WILLIAM MTITU

Nilipata taarifa kama saa sita hivi (usiku), nikaenda pale (nyumbani kwa Kanumba) nikamkuta Ray na wasanii wengi, lakini Kanumba alikuwa amelala macho yake yako juu.
Nilisikitika sana na bado nasikitika kwa hakika siamini mpaka sasa. Kumbuka Kanumba ni msanii mkubwa, kafanya kazi nyingi nzuri hata tulipofika Muhimbili tulikuwa watu wengi wamefika pale.
(Baadhi ya) manesi na madaktari walishindwa kufanya kazi wakaja pale mochwari kushuhudia, wasanii wa muziki na watu wengine wengi tu. Tukio lilikuwa la kusikitisha sana, Kanumba alikuwa amevaa pensi yake, amechana nywele. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba Kanumba hajaacha familia.
IVON SHERRY ‘MONALISA’

Kanumba alikuwa mmoja wa rafiki zangu wa karibu. Nimeumia sana. Nitaadhirika. Tulishaanza kufanya kazi za nje za kimataifa na tulitakiwa tukafanye filamu Ghana mwaka huu.
MOHAMED FRANK

Wakati tunaanza Kaole Sanaa Group mwaka 2002-2003, Kanumba alikuwa rafiki yangu wa karibu alipofanikiwa, hakuwasahau wasanii wenzake.
Nilipopata taarifa ya kifo chake sikuamini. Nilimwambia Dino, mbona siku ya wajinga imeshapita. Sikuamini kwa sababu siku moja niliwahi kupokea ujumbe ukisema Tino amefariki wakati si kweli. Dino akanisisitizia kwamba Kanumba amefariki. Ilinibidi nifunge safari moja huo huo hadi nyumbani kwake Sinza.
Kanumba atabaki kuwa Kanumba. Kifo chake ni pigo kubwa. Hakuna msanii anayeweza kuziba pengo lake. Tunapaswa kumshukuru Mungu. Siku zake za kuishi hapa duniani zimefikia mwisho.
Ameondoka akiwa kijana mdogo sana. Umri wake ni miaka 28. Ni juzi juzi tu alitengeneza filamu inayoitwa Ndoa yangu. Sijui alitaka kueleza nini katika filamu hiyo. Ni kama drama, lakini ndio ukweli wenyewe.
SANDRA

Kanumba alikuwa rafiki yangu sana. Tulipokuwa Kaole, alizoea sana kunitania. Siku moja aliniambia ‘Dada Sandra, nampenda sana yule mwanamke (msanii mwenzao), lakini naogopa kumwambia kwa sababu sina pesa.’ Alikuwa mtu wa utani sana.
ADAM SWEBE

Tumempoteza mtu aliyefanya mambo makubwa na ambayo hayawezi kusahaulika katika tasnia ya filamu. Na bado alikuwa na ndoto ya kufanya mambo mengi zaidi. Kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya filamu.
THEA

Huu ni msiba mkubwa na umetushua. Najiuliza kwa nini Kanumba.
IRENE UWOYA

Siwezi kumsahau Kanumba katika maisha yangu. Amenisaidia sana katika fani ya filamu. Kifo chake ni pigo kubwa sana kwangu na watanzania wote. Tumempoteza mtu muhimu.
UGONE MPHEHO

Ulikuwa mtu mbele ya watu, Ukajivika tabasamu cheko na bashasha,Ulikuwa wa mwanzo na jemadari, Kuona mbele na safari kuongoza,Ulikuwa wa mwisho kununa, Ulipokisimangwa kwa kero na ujuvi,Wewe ulishika panga, ukaingia mwituni na njia kutupasulia!Eh jiti kuu la mwituni, ndege wema na wabaya watamiapo,Eh mzizi ulotambaa, ukagusa nyika na bahari kwa pamoja,Eh mbuyu wa thamani, dawa poa na sumu kali zote zipo,Eh wimbo wa pozeo, jua la kuchea na na mwezi wa kuchwea.Nikwambe nini jabali, ulobeba tasnia,Nikusifuje kwa hili, mbinguni wakasikia,Leo dunia hulali, Pepo yakutazamia,













No comments:

Post a Comment