KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 18, 2012

ALLY CHOKI: Situmii uchawi kuvuta mashabiki



Akiri kutokuwa na uhusiano mzuri na Asha Baraka
Asema hanywi pombe wala kutumia dawa za kulevya

Aziponda tuzo za Kili
KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, Ally Choki amekiri kuwa, baadhi ya bendi zimekuwa zikitumia uchawi ili kuvuta mashabiki
Choki amekiri pia kuwa, ugonjwa wa ukimwi umesambaratisha maisha ya wanamuziki wengi kutokana na kuendekeza starehe na kutochukua tahadhari.
Mwanamuziki huyo wa zamani wa bendi za Twanga Pepeta, Achigo, Bantu Group, TOT Plus na Mchinga Sound, alisema hayo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
Choki alisema zipo baadhi ya bendi, ambazo hazipigi kwenye kumbi fulani kutokana na kuwepo kwa imani za ushirikiana na hata wanamuziki wake hawasaidiani kwa sababu ya imani hizo.
“Mimi situmii mambo ya uchawi, lakini upo na baadhi ya bendi zinafanya hivyo ili kuvutia mashabiki,”alisema.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mtangazaji wa kipindi hicho, Salama Jabir aliyetaka kujua iwapo ni kweli baada ya maonyesho viongozi wa bendi hukusanya vitu fulani ukumbini kwa lengo la kuvifanyia ushirikina.
Choki alisema binafsi hana tatizo na viongozi wa baadhi ya bendi alizowahi kupigia, lakini alikiri kuwa kwa sasa hana maelewano mazuri na mmiliki wa bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka.
“Tatizo la mama yetu Asha hajui kwamba kila mwanamuziki anahitaji kuwa na maisha mazuri hivyo kuhama kutoka bendi moja kwenda nyingine ni sehemu ya maisha,”alisema.
Mwimbaji huyo mwenye kipaji na mvuto alikiri pia kuwa, utumiaji wa dawa za kulevya umekuwa ukiwaathiri wanamuziki wengi nchini japokuwa wengi wanaofanya hivyo ni kwa sababu yah obi.
Alisema binafsi hajawahi kutumia dawa hizo, lakini aliwahi kunywa pombe miaka kadhaa iliyopita kabla ya kuamua kuacha baada ya kuona haina faida kwake.
“Kama ni kuvuta unga, ningeuvuta nilipokuwa naishi Kinondoni kwa sababu nilikuwa naishi karibu na nyumba ya wavuta unga, lakini sikuthubutu kufanya hivyo kutokana na kutambua athari zake,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu athari ya ukimwi kwa wanamuziki, Choki alikiri kuwa, ugonjwa huo umepoteza maisha ya wanamuziki wengi kutokana na ugonjwa huo kwa sababu ya kuendekeza starehe.
Choki alisema pia kuwa, baadhi ya wanamuziki walishindwa kujipanga vyema kwa ajili ya maisha yao ya baadaye na pale waliposhtuka, walijikuta wakiwa na familia kubwa na hivyo kushindwa kuzihudumia inavyotakiwa.
Kiongozi huyo wa Extra Bongo alisema hakuna tukio lililowahi kumshtua na kumuhuzinisha katika maisha yake kama vifo vya wasanii 13 wa kundi la taarabu la Five Stars vilivyotokana na ajali ya gari iliyotokea mwaka jana mkoani Morogoro.
Alisema kabla ya ajali hiyo, alikuwa na mpango wa kurekodi wimbo na mwimbaji Zena Hamisi wa kundi hilo na alizungumza naye kwa simu siku moja kabla ya ajali hiyo akimkumbusha kuhusu azma yake hiyo.
“Nikaja kushtuka kesho yake baada ya kupigiwa simu na kuelezwa kuwa, wanamuziki wote wa Five Stars wamekufa katika ajali ya gari. Muda huo huo nikampigia simu Zena kwa bahati nzuri akapokea, lakini alikuwa akilia kwa sababu walikuwa bado wapo eneo la ajali,”alisema.
Mwanamuziki huyo alisema maisha ya wanamuziki siku zote yapo hatarini kutokana na kusafiri mara kwa mara mikoani na kuongeza kuwa, hata bendi yake iliwahi kunusurika katika ajali ya gari iliyotokea mapema mwaka huu mkoani Iringa.
Choki alisema hapendezwi na tabia ya baadhi ya mapedeshee kupenda kuwatongoza wanawake wanaocheza shoo katika bendi mbalimbali za muziki nchini.
Alisema hawezi kuruhusu tabia hiyo katika bendi yake na aliwaita mapedeshee hao kuwa ni watu wasiojiamini.
Mwimbaji huyo nguli alisema kamwe hawezi kuyasahau matukio matatu makubwa yaliyomtokea alipokuwa katika bendi ya Twanga Pepeta. Aliyataja matukio hayo kuwa ni yale ya kuingia kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee kwa kutumia farasi, ngamia na kijiko.
Alisema tukio la kuingia ukumbini kwa farasa lilikuwa na mvuto zaidi kwa sababu mnyama huyo alimwangusha sakafuni baada ya shabiki mmoja kujaribu kupita katikati ya miguu yake.
Choki alisema pia kuwa, tukio la kuingia ukumbini na ngamia nalo lilikuwa na vioja kwake kwa sababu mnyama huyo aligoma kuendelea na safari baada ya kusikia kelele za mashabiki ukumbini.
Mwanamuziki huyo alisema katika maisha yake, anachukizwa na maneno ya uongo kwa sababu yanaweza kumweka mtu kwenye wakati mgumu kimaisha na hata kupoteza maisha yake kwa kihoro.
Akizungumzia tuzo za muziki za Kilimanjaro, Choki alisema aliamua kujitoa kuanzia mwaka jana baada ya kubaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa na pia kutokuwa na mwelekeo mzuri.
Akifafanua, alisema upangaji wa tuzo hizo ni mbovu kutokana na waandaaji kuwashindanisha wasanii wanaopiga aina tofauti ya muziki.
“Huwezi kumshindanisha Khadija Kopa na Shaa au Mzee Yusuph na Diamond kwa sababu muziki wanaopiga ni tofauti na wao wenyewe ni vizazi tofauti.
“Pia huwezi kunishindanisha mimi na Mzee Gurumo kwa sababu ni vizazi tofauti. Kila aina ya muziki inapaswa kuwa na tuzo zake,”alisisitiza.

No comments:

Post a Comment