KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, April 18, 2012

BANZA: Sina mkataba na Extra Bongo

MTUNZI na mwimbaji mahiri wa nyimbo za muziki wa dansi nchini, Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ amefichua kuwa, hana mkataba na bendi ya Extra Bongo.
Banza amesema amekuwa akifanyakazi katika bendi hiyo kiurafiki, kutokana na makubaliano waliyofikia kati yake na kiongozi wa Extra Bongo, Ally Choki.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Banza alisema aliamua kujiunga na Extra Bongo kwa vile hakuwa na bendi ya kudumu.
“Choki alinifuata, akaniambia ‘Banza kwa sasa huna mahali, ambako watu wakikutafuta, watakupata. Njoo ujiunge nami Extra Bongo’ nami nikaona ni kweli, nikakubali,”alisema.
“Nilikuwa sina mahali pa kudumu, nilikuwa nahangaika, nikaamua nifanyekazi na Choki na nipo Extra Bongo hadi sasa,”aliongeza mwanamuziki huyo wa zamani wa Twanga Pepeta International.
Banza aliutetea uamuzi wake huo kwamba hauna tatizo kwa vile yeye na Choki ni marafiki na kwamba hata katika maslahi yake, hawezi kumdhulumu.
Mtunzi na mwimbaji huyo mwenye kipaji aliwahi kutamba katika bendi mbalimbali nchini, zikiwemo TOT Plus, Bambino Sound na Rufita.
Mbali na kuimba nyimbo za muziki wa dansi, Banza pia anao uwezo wa kuimba nyimbo za taarab. Kibao chake cha kwanza cha muziki huo kinajulikana kwa jina la ‘Wamezoea kusema’.
Kwa sasa, Banza anajiandaa kurekodi kibao kingine cha muziki huo, akisaidiwa na kiongozi msaidizi wa Mashauzi Classic, Thabiti Abdul.

No comments:

Post a Comment