KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

MAMA KANUMBA: Nipo tayari kumsamehe Lulu

Mama mzazi wa msanii Steven Kanumba, Flora Mutegoa amesema
yupo tayari kumsamehe msanii Elizabeth Michael 'Lulu',
anayetuhumiwa kumuua Kanumba iwapo vyombo vya sheria
vitamuona hana hatia hiyo.
Flora pia alikanusha madai kuwa, marehemu Kanumba
alikorofishana na baba yake ndiyo sababu hakuweza kushiriki
katika mazishi ya mtoto wake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu
Kanumba, Sinza mjini Dar es Salaam, Flora alisema taarifa hizo
hazina ukweli wowote.
"Marehemu Kanumba na baba yake walikuwa na uhusiano mzuri
isipokuwa watu waliipokea tofauti filamu aliyoitoa, ambayo ilikuwa
ikielezea maisha yake. Hata mimi sijui baba yake aliipokea
vipi,"alisema.
Bi Flora aliishukuru serikali na wananchi waliojitokeza katika
mazishi ya mwanaye na kuongeza kuwa, hakutarajia iwapo
angezikwa na watu wengi kiasi kile.
Aliongeza kuwa, Kanumba na baba yake hawakutofautiana kama
inavyodaiwa na baadhi ya watu, isipokuwa anachojua ni kwamba
mtoto wake aliamua kuwa mbali na mzee ili kujitafutia maisha
yake.
Alisema Mzee Charles Kanumba alishindwa kuhudhuria mazishi ya
mwanaye kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya miguu,
ambayo yamempata uzeeni.
"Kwa kweli sina cha kusema zaidi ya kutoa shukurani zangu za
dhati kwa serikali na watu wote wakiwemo wasanii wenzake, hivi
sasa tunaendelea na mambo ya kifamilia,"alisema.
Alipoulizwa ameupokeaje msiba wa mtoto wake, Bi Flora alisema
kifo chake hakina tofauti na vifo vingine na kusisitiza kuwa, kila
binadamu lazima afe.
"Kama familia, tupo tayari kupokea taarifa zozote, ambazo
tutapewa na vyombo husika, daktari aliyeuchunguza mwili wake
pamoja na polisi, ambao bado wanaendelea na uchunguzi. Kwa
sasa siwezi kusema mengi, naiachia serikali ifanyekazi
yake,"alisema.
Mama Kanumba pia alikanusha madai kuwa, kijana wake ameacha
mtoto. Alisema anachofahamu ni kwamba, mwanaye alikutwa na
mauti akiwa hajaoa na wala hakuwahi kupata mtoto.
Alisema marehemu Kanumba ni mtoto pekee aliyezaa na baba
yake, lakini anao watoto wengine wawili aliozaa na mwanaume
mwingine.

No comments:

Post a Comment