KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

LULU ABURUZWA KORTINI

MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael, maarufu kwa jina la Lulu, amepandishwa kizimbani kujibu shitaka la mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Lulu (18) alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Agustina Mbando na kusomewa shitaka linalomkabili.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Elizabeth Kaganda akisoma hati ya mashitaka, alimtaja Lulu kuwa ana miaka 18, lakini alikana na kudai umri wake ni miaka 17.
Elizabeth alidai, Aprili 7 mwaka huu, eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam, mshitakiwa alimuua Kanumba.
Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shitaka hilo.
Elizabeth alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na aliomba tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 23 mwaka huu.
Wakati msanii huyo akifikishwa mahakamani hapo, alikuwa amepakiwa kwenye gari lenye namba T 848 BNV aina ya Suzuki na kwenye vioo vyake lilikuwa na namba PT 2565 huku likisindikizwa na gari la polisi.
Kulikuwepo na usiri mkubwa baina ya watu waliomfikisha mahakamani msanii huyo, ambao walionekana kutotaka watu wengine, hasa waandishi wa habari wafahamu juu ya suala hilo.
Hali hiyo ilisababisha askari hao kufika mahakamani hapo wakiwa katika magari mawili tofauti huku moja, lililombemba likiwa mbele aina ya Toyota Rav 4 lenye namba za usajili T 848 BNV huku likiwa na rangi nyeupe na vioo vyake vikiwa na rangi nyeusi.
Gari hilo liliwasili mahakamani hapo saa tatu asubuhi kwa nyuma likisindikizwa na Defender lenye namba PT 1848 lililokuwa na askari wanne waliobeba silaha.
Licha ya kuwasili kwa magari hayo, hakuna mwandishi au makarani wa mahakama hiyo,walioweza kufahamu iwapo alikuwemo kwenye msafara huo.
Hilo lilitokana na staili iliyotumiwa na askari hao kwa kuwaacha mbali kabisa askari wa ulinzi waliokuwa wanaongozana na gari lililombeba, ambalo lilizunguka nyuma ya mahakama hiyo kwenda kumshusha na kumuingiza kwenye chumba cha mahakama.
Lulu alikuwa ameambatana na askari kanzu wa kike wawili waliomuweka katikati huku wakionekana kama watu wanaozungumza jambo fulani, ambalo kwa mtu wa kawaida asingeweza kutambua kilichokuwa kikiendelea kati yao.
Askari hao waliingia naye hadi chumba cha mahakama na kumuacha kwenda kukaa katika benchi lililokuwepo katika chumba hicho.
Wakati Lulu anakwenda kukaa kwenye benchi, alionekana kutokuwa na wasiwasi wowote kwani alikuwa akitembea kwa madaha huku akiwa amevaa mavazi nadhifu. Alivaa dira jeupe na kiremba cha rangi ya pinki.
Kupandishwa kizimbani kwa msanii huyo, kumeanzisha safari mpya ya maisha ya msanii huyo, aliyejizolea sifa nyingi kutokana na kuigiza filamu mbalimbali zilizompatia sifa kemkem.
Marehemu Kanumba alizikwa juzi kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam baada ya maiti yake kuagwa na viongozi mbalimbali wa serikali, ndugu na marafiki kwenye viwanja vya Leaders.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela amesema hawajui kwa nini Lulu ameamua kudanganya umri wake kwani katika maelezo yake aliyoandika polisi, alidai ana umri wa miaka 18.
Kamanda huyo alisema walifanikiwa kupata cheti chake cha kuzaliwa, ambacho kinaonyesha kuwa, atafikisha umri huo mwakani. Kwa sasa, umri wa Lulu ni miaka 17.
“Tunafahamu kwamba kwa kupitia maelezo yake aliyoandika polisi, amedai ana umri wa miaka 18, lakini hatufahamu kwa nini amedanganya kwani ni tofauti na cheti chake cha kuzaliwa, ambacho kinaonyesha ana miaka 17,” alisema Kenyela.
Akizungumzia kuhusu Lulu kupelekwa hospitali ya Mwananyamala, Kamanda Kenyela alisema ni haki ya kila mtuhumiwa, hasa wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa kama ya mauaji kupimwa afya zao.
Alisema walimpeleka Lulu hospitali kwa ajili ya kupimwa afya yake kama nzuri na kwa kuzingatia kulikuwa na ugomvi. Pia alisema katika uchunguzi huo, lazima apimwe akili yake na afya yake.
Lulu alifikishwa kwenye hospitali hiyo kwa mara ya kwanza kwanza Jumapili iliyopita saa 11.00 jioni akiwa chini ya ulinzi wa askari zaidi ya watano.
Polisi waliamua kumfikisha Lulu hospitali baada ya kulalamika kuwa anaumwa na kujisikia vibaya. Alifikishwa tena kwenye hospitali hiyo kwa mara ya pili juzi.
Habari kutoka kwa baadhi ya madaktari waliompokea zimeeleza kuwa, msichana huyo hakuonyesha kuwa na wasiwasi wowote na alipoulizwa sababu ya kujisikia vibaya, alidai ni kutokana na kugombana na mpenzi wake.
Kwa mujibu wa habari hizo, baada ya madaktari kumdadisi zaidi, Lulu alimtaja mpenzi wake huyo kuwa ni marehemu Kanumba, ambaye alifariki dunia Jumamosi iliyopita.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, baada ya Lulu kuona madaktari wakimshangaa kutokana na kutoonyesha wasiwasi wowote, aliwajibu kwamba tayari limeshatokea.

No comments:

Post a Comment