KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 9, 2012

MUHIMBILI YATOA RIPOTI KIFO CHA KANUMBA

Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamethibitisha kuwa, msanii nyota wa filamu
nchini, Steven Kanumba, amefariki kwa tatizo la mtikisiko wa ubongo unaojulikana
kitaalamu kama 'brain concussion'.'

Brain concussion' ni hali ya ubongo kushindwa kufanyakazi kwa muda kutokana na
mtu kuumizwa kichwa au kushikwa na kiwewe kikali.

Kwa mujibu wa magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti toleo la leo, taarifa za ndani zilizopatikana juzi kutoka kwa jopo la madaktari bingwa watano walioufanyia uchunguzi mwili wa Kanumba,zinaeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa.

Mmoja wa madaktari hao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye hakutaka kutajwa
gazetini kwa kuwa si msemaji, alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia
uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.

"Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia muda wa saa nne asubuhi
hadi saa saba kasoro za mchana na tukagundua kuwa, marehemu alifariki kutokana
na mtikisiko wa ubongo, kwa kitaalamu brain concussion,"alisema.

Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo alizungumza kwa ufupi kuwa,
waligundua kwamba ubongo ulikuwa umevimba na kushuka mpaka karibu na uti wa
mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji na ndiyo maana msanii huyo alikufa
pale pale.

Daktari wa awali alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo, ambao husababisha
kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure).

"Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya
nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka,"alisema daktari huyo.

Aliongeza kuwa, mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wa Kanumba.

Alisema:" Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndio maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji."

Aliongeza:" Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huwezo kutokwa na mapovu mdomoni na hukoropma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki."

Daktari huyo alisema, sehemu ya maono na majimaji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa mkemia mkuu ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo.

No comments:

Post a Comment