KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, April 28, 2012

TOTO: Tutaipa ubingwa Simba



KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Toto African ya Mwanza, Athumani Bilal ametamba kuwa, kikosi chake kitaisambaratisha Azam katika mechi yao ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa Jumatatu ijayo.
Bilali alisema kwa njia ya simu juzi kutoka Mwanza kuwa, wanakuja Dar es Salaam kwa lengo la kuzoa pointi zote tatu kutoka kwa Azam ili wajinusuru katika janja la kushuka daraja.
Kocha huyo alisema hadi sasa hawajawa na uhakika wa kubaki katika ligi kuu, hasa iwapo watapoteza mechi hiyo dhidi ya Azam na ile ya mwisho dhidi ya Coastal Union itakayochezwa mjini Tanga.
Pambano kati ya Toto African na Azam linasubiriwa kwa hamu kubwa kwa vile ndilo litakaloamua iwapo Simba inaweza kutangaza ubingwa mapema au la.
Simba ilikuwa itangaze ubingwa Jumatatu iliyopita iwapo pambano kati ya Azam na Mtibwa Sugar lingemalizika kwa sare, lakini lilivunjika dakika ya 88 baada ya Mtibwa kugomea penalti. Hadi pambano hilo lilipomalizika, timu hizo zilikuwa sare ya bao 1-1.
Kwa mujibu wa kanuni, hatma ya pambano linalovunjika itasubiri ripoti ya mwamuzi na kamishna, itakayowasilishwa kwa kamati ya ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Simba hadi sasa inazo pointi 59 na iwapo itashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Yanga, itakuwa na pointi 62, ambazo haziwezi kufikiwa na timu zingine.
Lakini iwapo Simba itafungwa na Yanga, itabaki na pointi 59, ambazo zinaweza kufikiwa na Azam kama itapewa ushindi katika mechi yake dhidi ya Mtibwa na kushinda mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Toto na Kagera Sugar.
“Matumaini yetu ya kufanya vizuri dhidi ya Azam ni makubwa. Kama tuliweza kuibana Simba na kutoka nayo sare kabla ya kuifunga Yanga, hatuoni kwa nini tushindwe kufanya hivyo kwa Azam,”alisema.
Bilali alisema hawataki kufanya makosa yaliyoifanya timu hiyo ichapwe bao 1-0 na Kagera Sugar mwishoni mwa wiki iliyopita na kuongeza kuwa, wameweza kurekebisha dosari zilizojitokeza katika mechi hiyo.
Iwapo Toto itaifunga Azam ama kutoka nayo sare, itakuwa imeipa ubingwa Simba kwa vile wapinzani wao hata kama watapewa ushindi dhidi ya Mtibwa na kuifunga Kagera, hawataweza kufikisha pointi 59.
"Pambano hili kwetu ni sawa na vita ya kuhakikisha tunabakia kwenye ligi kuu msimu ujao, lakini jambo la msingi kwa vijana wangu ni kucheza soka ya kiwango cha juu na waamuzi kuzingatia sheria 17 za soka,”alisisitiza.

No comments:

Post a Comment