KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 5, 2012

Wachezaji Yanga wapunguziwa adhabu



Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesikitishwa na
vitendo vilivyofanywa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo namba 132 wa
Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yao na Azam uliofanyika Machi 10 mwaka huu.


Vilevile imesikitishwa na uongozi wa klabu ya Yanga kushindwa kuvikemea hadharani
vitendo hivyo vilivyofanywa na wachezaji wake.

Kamati hiyo ilikutana jana (Aprili 4 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Kamishna
mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana kujadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Yanga
kupinga uamuzi uliofanywa na Kamati ya Ligi ya TFF dhidi ya wachezaji hao.

Mbele ya Kamati hiyo, Yanga ilikuwa na rufani mbili. Rufani ya kwanza ya Machi 11
mwaka huu iliomba matokeo ya mchezo huo yafutwe, ikiwemo kadi walizooneshwa
wachezaji wao na mwamuzi aadhibiwe kwa kushindwa kumudu mchezo huo.

Wakati ikifanya mawasilisho (submissions) mbele ya Kamati, Yanga iliamua kuondoa
rufani hiyo kwa vile katika ya pili iliyokatwa Machi 14 mwaka huu ikipinga adhabu
zilizotolewa ina kifungu (j) kilichodai Kamati ya Ligi ya TFF ilikosea kutotoa uamuzi
wowote kwa refa aliyedaiwa kutoa maneno ya kashfa na kejeli kwa wachezaji wao.

Baada ya kusikiliza submissions za pande zote mbili (walalamikaji- Yanga) ambao
walikiri hatia ya vitendo hivyo na kuomba wachezaji wake wapunguziwe adhabu, na
(walalamikiwa- TFF), Kamati imetoa uamuzi ufuatao;

Mchezaji Nurdin Bakari amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu za ligi na faini ya
sh. milioni moja. Omega Seme amepewa adhabu ya kutocheza mechi tatu na faini ya
sh. milioni moja.

Nadir Haroub atatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ambayo haikatiwi rufani.

Lakini Kamati ya Nidhamu imeondoa adhabu ya mechi nyingine tatu iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa vile hizo atazitumikia kwa pamoja, lakini adhabu ya faini ya sh. 500,000 inabaki, hivyo atalipa jumla ya sh. milioni moja.

Stephano Mwasika ambaye alifungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja,
adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za msimu wa ligi
2011/2012, lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili.

Kwa upande wa Jerryson Tegete aliyefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000,
adhabu yake imebadilishwa na sasa atakosa mechi zilizobaki za ligi msimu huu
(2011/2012), lakini faini imeongezwa na kuwa sh. milioni mbili. Adhabu ya Yanga kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake inabaki kama ilivyo kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1).

Vilevile adhabu ya faini ya sh. 500,000 kutokana na timu hiyo kupata kadi tano na kuendelea kwenye mechi moja inabaki kama ilivyo vile kanuni ya 25(1) haikatiwi rufani. Kamati imesema adhabu zimeanza kutumika tangu zilipotolewa na Kamati ya Ligi, hivyo kwa ambapo tayari wameshatumikia mechi kadhaa zinahesabika.

Kwa watakaoshindwa kulipa faini wataendelea kuwa nje ya uwanja mpaka fedha hizo zitakapolipwa.

Mwenyekiti Tibaigana amewataka viongozi wa Yanga kusimamia nidhamu ya wachezaji wao, na makosa hayo yakijirudia adhabu kali zaidi zitatolewa. Pia Kamati ya Nidhamu ya TFF haikujadili suala la Yanga kunyang’anywa pointi tatu katika mchezo kati yake na Coastal Union kwa vile hakukuwa na rufani hiyo mbele yake.

No comments:

Post a Comment