KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, April 9, 2012

RATIBA YA MAZISHI YA KANUMBA

Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa
jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa
leo makaburi ya Kinondoni, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu,
mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya
wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda
wote wa Afrika Mashariki na Kati.
Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi
ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo
kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye
shughuli nzima.
RATIBAMwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka
Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa
Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa
ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote
kumuaga.
Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga
kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima
mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.
Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa
na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa
atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed
Gharib Bilal.
Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00
kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.Saa 6:00 mchana, ratiba ya
kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati
wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni,
msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea
makaburini.Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya
marehemu.
Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu
yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.Utulivu, unyenyekevu na
ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga
mpendwa wetu Kanumba.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee
kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua.
Jina lake lihimidiwe.
K.N.Y GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

No comments:

Post a Comment