KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

SYKES: Ni vigumu kuziba pengo la Kanumba

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Dully Sykes amesema itachukua muda mrefu Tanzania kumpata mcheza filamu atakayeweza kuziba pengo la marehemu Steven Kanumba.
Akizungumza kwa njia ya simu mjini Dar es Salaam jana, Sykes alisema Kanumba alikuwa msanii mwenye kipaji cha aina yake ndio sababu alikuwa kipenzi cha watanzania wengi.
Sykes alisema katika kipindi chote cha uhai wake, Kanumba alikuwa na ushirikiano mkubwa na wasanii wenzake na pia alipenda kuwasaidia.
“Kusema ule ukweli, kifo chake ni pigo kubwa na ni pengo, ambalo sidhani kama linaweza kuzibika ama itachukua muda mrefu kuliziba,”alisema.
Aliongeza kuwa, kutokana na umahiri wake katika utengenezaji wa filamu, marehemu Kanumba aliweza kulitangaza vyema jina la Tanzania kimataifa kupitia fani ya filamu.
Sykes alisema kujitokeza kwa maelfu ya watu wakati wa mazishi yake ni uthibitisho wa wazi kwamba, msanii huyo alikuwa mtu wa watu na kipendi cha watanzania.
“Sijawahi kumsikia mtu akimzungumza Kanumba kwa mabaya, na kama ilitokea hivyo, basi ni watu wachache. Alipendwa na kila mtu,”alisisitiza.
Sykes aliwataka wasanii wa fani mbalimbali nchini kumuenzi Kanumba kwa kuonyesha upendo miongoni mwao na kusaidiana kwa hali na mali wakati wote wa maisha yao.
Alisema iwapo wasanii watajiheshimu na kuwaheshimu wenzao, itakuwa ni rahisi kwa mashabiki nao kuwafurahia na kuwaenzi kwa kujitokeza kwa wingi kuwazika kama ilivyotokea kwa Kanumba.

No comments:

Post a Comment