KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 12, 2012

KANUMBA NDIYE ALIYEFUFUA EXTRA BONGO-CHOKI

MKURUGENZI na mwimbaji wa bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, Ally Choki amesema, daima atamkumbuka mwigizaji filamu nyota nchini, Steven Kanumba aliyezikwa juzi, kwa sababu ndiye aliyemshauri kuifufua bendi ya Extra Bongo.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa jana kufuatia kifo cha msanii huyo kilichotokea Ijumaa iliyopita nyumbani kwake Sinza Vatican, Dar es Salaam, Choki alisema msiba huo umempa simanzi kubwa na siku alipopata habari hiyo hakuamini.
“Nilipoambiwa Kanumba kafariki, sikuamini na usiku ule ule nilikwenda Muhimbili kujionea mwenyewe. Nimeumia sana, Kanumba alikuwa rafiki yangu na kuna wimbo tuliwahi kuimba pamoja katika mtindo wa zing zong,” alisema Choki.
Alisema anamkumbuka zaidi msanii huyo wa filamu aliyetamba ndani na nje ya nchi kwani, ndiye alimshauri kuifufua bendi ya Extra Bongo baada ya kusambaratika miaka kadhaa iliyopita.
Choki alisema Kanumba aliwakutanisha na mfanyabiashara Chief Kiumbe katika hoteli ya Lamada na kuzungumza kwa kina juu ya umuhimu wa kuirudisha Extra Bongo na mazungumzo hayo yalizaa matunda.
“Kwa hiyo unampotaja Kanumba, naona mtu muhimu kwangu. Alinishauri nianze kujitegemea badala ya kuajiriwa na wazo hilo liliniingia, nikairudisha bendi yangu,” anasema Choki aliyewahi kuimba katika bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Mchinga Generation ‘Timbatimba’ na TOT Plus. Nyota huyo wa muziki wa dansi alisema, kitu kingine kinachomsikitisha baada ya kifo cha Kanumba ni kutomuona tena msanii huyo kama ilivyokuwa zamani, ambapo walikuwa wanabadilishana mawazo na kula pamoja mchana kwa sababu ya ukaribu wa ofisi zao zilizopo Sinza, Dar es Salaam.
Choki ameishauri serikali kuwa na utaratibu maalumu wa kuchukua majukumu ya misiba ya watu mashuhuri kama Kanumba kwa sababu kutasaidia wasanii kupewa heshima.
“Serikali ifanye hivi kwa wanamuziki, waigizaji filamu na watu wa sanaa nyingine. Itazame umashuhuri wao na kubeba jukumu la msiba ili kuwapa heshima wasanii,” alisema Choki.
Akitolea mfano, alisema kamati ya maandalizi ya mazishi, ambayo Choki alikuwa mjumbe, ilijitahidi kuratibu shughuli za msiba wa msanii huyo, lakini imeacha manung’uniko kwa Watanzania wengi waliopenda kushiriki katika maziko.
Alisema watu wengi walipenda kuaga mwili wa Kanumba na ilishindakana kutokana na umati uliojitokeza kwenye viwanja vya Leaders Club kuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa na kamati.
“Umati ule umenishangaza sana na umeonyesha jinsi gani Kanumba alivyokuwa anapendwa. Na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa serikali kujitwisha jukumu kwa kuwa watu wanasema mwili ungeagwa siku mbili katika Uwanja wa Taifa,” aliongeza Choki.

No comments:

Post a Comment