KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 26, 2012

Ndolanga, El-Maamry watunukiwa urais wa heshima TFF


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewatunikia urais wa heshima wenyeviti wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Alhaji Muhidin Ndolanga na Said Hamad El-Maamry.
Uamuzi wa TFF kuwapa heshima hiyo Ndolanga na El-Maamry ulifikiwa wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Water Front mjini Dar es Salaam.
Akifungua mkutano huo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema wamefikia uamuzi huo kutokana kuheshimu kazi nzuri iliyofanywa na viongozi hao walipokuwa wakiiongoza FAT.
"Tulishazungumza siku za nyuma kwenye mkutano kama huu kwamba tutakuwa tunatoa nyadhifa za heshima kwa watu, ambao mchango wao unaonekana na unathaminiwa kwenye tasnia ya soka. Hivyo kwa kuanzia, tunawapa Ndolanga na El Maamry urais wa heshima wa TFF," alisema.
Tenga alisema wakati wakiwa viongozi wa FAT, Ndolanga na El Maamry walifanya kazi kwa ari na kujituma na hatimaye kuiletea Tanzania mafanikio makubwa kisoka.
Rais huyo wa TFF alisema anaamini, heshima hiyo itawafanya Ndolanga na El-Maamry waongeze moyo wa kujituma na kusaidia kukuza soka ya Tanzania kila watakapohitajika kufanya hivyo.
Tenga alisema kwa sasa Ndolanga ni mjumbe wa heshima katika Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki (CECAFA) wakati El-Maamry ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Akizungumza baada ya kutunukiwa heshima hiyo, El Maamry aliishukuu TFF kwa kutambua na kuthamini kazi alizofanya wakati wa uongozi wake.
"Leo nimefarijika na nina furaha kubwa kwani hata nyumbani sasa wamekubali na wamethamini mchango wangu kwenye soka ya Tanzania. Kuna msemo unaosema 'Nabii havumi kwao,' lakini sasa umekuwa tofauti, ndiyo maana nimepewa urais wa heshima wa TFF," alisema.
  Kwa upande wake, Ndolanga alisema amefurahishwa na heshima aliyopewa na kuwataka viongozi wa vyama vya mikoa, klabu na TFF kuendelea kumtumia Tenga katika kuboresha soka ya Tanzania kwa sababu bado anahitajika kwa kiasi kikubwa.
"Mara nyingi tumezoea kuwatunuku tuzo za heshima kama hizi watu waliokufa, lakini naishukuru sana TFF kwa kuamua kunipa heshima hii wakati nikiwa hai kwani binafsi imenifurahisha kwa vile inaonyesha ni jinsi gani nilivyochangia kuinua soka yetu," alisema.
Ndolanga pia aliwataka viongozi wa vyama vya soka vya mikoa kuhakikisha kuwa, soka inachezwa katika mikoa yote nchini badala ya kuuacha mkoa wa Dar es Salaam pekee ukitamba katika mchezo huo.
Katika hatua nyingine, TFF imesema fedha ilizoahidi kuvipatia vyama vya soka vya mikoa na vyama shirikishi vya shirikisho hilo, zitaanza kutolewa kesho.
Tenga alisema jana kuwa, fedha hizo zitatolewa kwa njia ya hundi na lazima zitiwe saini na mwenyekiti pamoja na katibu wa chama husika. Alisema kila chama cha soka cha mkoa kitapatiwa sh. milioni mbili wakati vyama shiriki vitapatiwa sh. milioni moja.
Rais huyo wa TFF alisema fedha hizo zinapaswa kutumika kuandaa semina, kozi, kununulia samani za ofisi na kuendesha michuano ya vijana kwa lengo la kuinua viwango vya soka mikoani.

No comments:

Post a Comment