KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 28, 2013

SIOGOPI KUTIMULIWA-KESHI


LAGOS, Nigeria
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria, Stephen Keshi, amesisitiza kuwa, hana wasiwasi wa kutimuliwa kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia za 2014 zitakazofanyika Brazil.
Ikiwa chini ya Keshi, Nigeria ilifanikiwa kufuzu kucheza fainali za kombe hilo baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Ethiopia katika mechi za hatua ya mtoano.
Keshi, ambaye alikuwa nahodha wa Nigeria miaka 1980, aliwahi kuzikosa fainali za michuano hiyo mara mbili baada ya kuiwezesha nchi hiyo kufuzu kucheza kombe hilo.
Mwaka 2002, Keshi alikuwa msaidizi wa Shuaibu Amodu wakati Nigeria ilipofuzu kucheza fainali za kombe hilo, lakini makocha hao wawili walitimuliwa na nafasi yao ilichukuliwa na Adegboye Onigbinde. Fainali za mwaka huo ziliandaliwa kwa pamoja na Korea Kusini na Japan.
Miaka minne baadaye, Keshi alipatwa na mkasa mwingine unaofanana na huo baada ya Chama cha Soka cha Togo kumtimua, licha ya kuiwezesha nchi hiyo kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2006 zilizofanyika Ujerumani.
Keshi (51) ameelezea msimamo wake huo siku chache baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF), kinafanya mipango ya kuajiri kocha mzungu kwa ajili ya fainali za Brazil.
"Kazi hii ni ya kuajiriwa na kutimuliwa,"amesema Keshi. "Wakati nilipotimuliwa 2002, nilipatwa na mshtuko, lakini ndivyo maisha yalivyo. Sote tunaendelea na maisha kwa sababu huwezi kuendelea kuishi kwa hasira na kukata tamaa."
"Tunazungumzia Nigeria hapa, hivyo huwezi kujua nini kinaweza kutokea. Lakini jambo la muhimu kwa sasa ni kwamba, tumeelekeza nguvu na akili zetu katika kile kilicho mbele yetu, ambacho ni kuwaandaa wachezaji, si kingine,"alisema kocha huyo.
Keshi alisema si jambo zuri kwa mtu kuisumbua akili yake juu ya kile kinachoweza kutokea. Alisema anashukuru amefanikisha kufanya kile, ambacho wengi hawakuwa na matarajio nacho na kwamba kazi hiyo inaendelea.
"Siwezi kuishi kwa woga wa kutimuliwa. Kiukweli, ni kupoteza nguvu,"alisisitiza.
Keshi amekuwa na uhusiano mbovu na waajiri wake,NFF, tangu alipokiongoza kikosi cha Nigeria, kilichokuwa kikiundwa na vijana wengi wapya, kutwaa ubingwa wa Afrika mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Kocha huyo na wasaidizi wake, wanadai mishahara ya miezi saba na Keshi amelipwa mishahara ya miezi miwili tu tangu alipoiongoza Nigeria kutwaa kombe hilo, ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1994.
 Mwanasoka huyo mkongwe ameielezea hali hiyo kuwa, inakatisha tamaa na haikubaliki na ameishutumu NFF kwa kushindwa kumlipa malimbikizo ya mishahara yake.
Waziri wa Michezo wa Nigeria, Bolaji Abdullahi amemshutumu Keshi kwa kulizungumza suala hilo kwenye vyombo vya habari.
Pamoja na kutolipwa mishahara yake, Keshi amesisitiza kuwa, ataendelea na kibarua chake cha kuinoa Nigeria na kujenga timu itakayofanya maajabu Brazil.
Amesema amestushwa na taarifa za maofisa wa NFF kutaka kuajiri kocha wa kigeni kwa ajili ya kumsaidia wakati wa fainali za Kombe la Dunia.
"Sihitaji msaada wa kocha wa kigeni, kuiongoza Nigeria kufanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia, hivyo kama kuna mtu anataka iwe hivyo, nitakataa ofa hiyo kwa sababu tayari ninao wasaidizi ninaofanyakazi nao,"amesema Keshi.

No comments:

Post a Comment