'
Thursday, November 21, 2013
BABU SEYA, PAPII KOCHA WAENDELEA KUSOTA JELA
JOPO la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, limeridhia hukumu ya kifungo cha maisha jela iliyotolewa kwa mwanamuziki Nguza Vicking 'Babu Seya' na mwanawe, Johnson Nguza 'Papii Kocha'.
Uamuzi wa jopo hilo la majaji, ulifikiwa leo kwenye mahakama hiyo baada ya kufanya mapitio ya hukumu hiyo.
Majaji watatu wakiongozwa na Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Massati, walisoma hukumu hiyo, ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na ndugu, jamaa na marafiki wa Babu Seya na Papii Kocha.
Babu Seya na mwanawe, waliwasilisha maombi ya mapitio hayo juu ya hukumu iliyotolewa Februari, mwaka 2010, na Jopo hilo la majaji, ambalo liliwatia hatiani kwa makosa ya ulawiti na ubakaji na kuwapa adhabu ya kifungo cha maisha.
Jopo hilo liliwaachia huru watoto wengine wa Babu Seya, Nguza Mbangu na Francis Nguza.
Oktoba 30, mwaka huu, wakati liliposikiliza hoja za kisheria kuhusu maombi ya mapitio zilizowasilishwa na wakili wa Babu Seya, Mabere Marando.
Mara baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, Babu Seya aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, ameamua kumuachia Mungu suala lao kwa sababu kwa Mungu hakuna makosa.
Kwa upande wake, Papii Kocha alisema kwa sasa wanategemea huruma ya Rais Jakaya Kikwete kwa vile mahakamani wamekwama.
Wakili Gabriel Nyela, aliyemwakilisha Marando alisema: "Hatua hii ni ya mwisho, hatuwezi kukata rufani sehemu nyingine."
Baada ya uamuzi huo wa mahakama, vilio vilisikika kutoka katika kila pembe, hasa vya akina mama, waliokuwa wakiwaonea huruma wanamuziki hao wawili.
Babu Seya na mwanawe wote wenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya kubaka na kuwalawiti watoto 10, kesi iliyosikilizwa kwa mara ya kwanza na kuhumumiwa kifungo cha maisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Juni 25, 2004.
Awali, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliwatia hatiani Babu Seya na wanawe watatu kwa jumla ya makosa 23 ya ubakaji na ulawiti walioshitakiwa nayo. Mashitaka 18 yalifutwa na uamuzi wa jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani. Washitakiwa walidaiwa kutenda makosa hayo, kati ya Aprili na Oktoba, 2003.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment