KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 21, 2013

MALINZI AIAHIDI ZFA UANACHAMA WA FIFA



Na Salum Vuai, Zanzibar

WIKI tatu tangu Jamal Malinzi achaguliwe kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana aliwasili Zanzibar na kufanya mazungunmzo na uongozi wa Chama cha Soka (ZFA), na kuahidi kulivalia njuga suala la kuipatia Zanzibar uanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

Katika mazungumzo hayo Malinzi alizungumzia suala la Zanzibar kupata uanachama wa FIFA  na CAF ambapo, alisema kuwa katika uongozi wake atahakikisha kuwa analishughulikia suala hilo, ili kuona kwa jinsi gani ataweza kulimaliza kwa Zanzibar kupata uanachama.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa VIP uwanja wa Amaan, Malinzi alisema katika kipindi chake cha uongozi TFF, atahakikisha  Zanzibar inapata uanachama wa FIFA  pamoja na ule wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kwa sasa, Zanzibar ni mwanachama shirikishi wa CAF, ambapo klabu zake zinazotwaa ubingwa wa ligi kuu na nafasi ya pili, huiwakilisha kwenye ligi ya mabingwa na Kombe la Shirikisho.
"Kwa kushirikiana na wenzangu TFF na ZFA, tutalishughulikia suala hilo ili kuona jinsi tunavyoweza kulimaliza kwa Zanzibar kupata uanachama wake FIFA na CAF," alieleza Rais huyo.
Malinzi alisema umefika wakati sasa ZFA ikawa na mwakilishi wake ndani ya Kamati Tendaji ya TFF, na kueleza kuwa, akisema atapeleka pendekezo katika kamati hiyo, ili kuifanyia marekebisho katiba ya shirikisho katika mkutano mkuu ujao.
Alifahamisha kuwa, marekebisho hayo yatafanyika kwa lengo la kuingiza kifungu kitakachoipa Zanzibar nafasi hiyo katika Kamati Tendaji ya TFF.
Kuhusu muundo wa timu za Taifa za Tanzania kwa wachezaji walio katika umri tafauti, Malinzi alisema hivi karibuni, kutafanyika kikao maalumu cha jopo la walimu wa michezo hapa Zanzibar, kwa lengo la kupanga mikakati ya kuimarisha timu hizo.
Kwa upande wa ligi ya Muungano ambayo imekufa kwa miaka mingi baada ya Zanzibar kupata nafasi ya kushiriki yenyewe  katika michuano ya CAF, alisema atahakikisha ligi hiyo inarudi tena japo kwa misingi mipya badala ya ile ya zamani.
Katika hatua nyengine, Rais huyo aliyerithi nafasi ya Leodgar Tenga aliyemaliza muda wake, alisema TFF hivi sasa iko katika mipango ya kuutumia utalii katika kuinua michezo, kwa kuwalika magwiji wa soka wa zamani pamoja na klabu maarufu duniani.
Itakumbukwa kuwa, miaka miwili iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Ali Juma Shamuhuna, aliongoza ujumbe mzito jijini Geneva, Uswisi kuiombea Zanzibar uanachama wa FIFA, lakini ombi hilo liligonga mwamba ikielezwa kuwa nchi hiyo haitambuliwi kimataifa kwa kuwa inabebwa na Tanzania kupitia TFF.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wote wa juu na wengine wa ZFA akiwemo Rais wake Ravia Idarous Faina.

No comments:

Post a Comment