KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 28, 2013

NYOTA 10 WAONGEZWA MIKATABA YANGA

KLABU ya Yanga imewaongezea mikataba ya muda mrefu, wachezaji wake nyota 10 na sasa wataendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2016.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kaziguto alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, uamuzi wa kuwaongezea mikataba wachezaji hao, umetokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.
Wachezaji walioongezewa mikataba ni Kelvin Yondani (2014-2016), Nadir Haroub 'Cannavaro' (2014-2016), Athumani Iddi 'Chuji' (2014-2016), Simon Msuva (2014-2016) na Jerry Tegete (2014-2016).
Wengine ni Saidi Bahanuzi, Salum Telela, David Luhende, Oscar Joshua na Didier Kavumbagu, ambao nao wameongezewa mikataba ya miaka miwili hadi 2016.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdalla Bin Kleb amesema, wachezaji hao ni baadhi ya waliomaliza taratibu zote za kutia saini mikataba mipya, itakayowafanya waendelee kuitumikia klabu hiyo kwa miaka miwili zaidi.
"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji wetu wengine na mazungumzo yanaendelea vizuri. Tunaamini muda si mrefu, nao tutakuwa tumeshamalizana nao ili waweze kuendelea kuitumika Yanga tena kwa muda mrefu, "alisema Bin Kleb.
Uamuzi wa Yanga kuwaongezea mikataba wachezaji hao, umekuja baada ya kuwepo na taarifa kwamba, baadhi ya klabu, ikiwemo Simba, zilianza kuwanyemelea baada ya kubaini kwamba mikataba yao inakaribia kumalizika.
Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Bora ulioko Mabatini-Kijitonyama kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Simba.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kaziguto alisema jana kuwa, kikosi hicho kinafanya mazoezi kikiwa chini ya kocha wake, Ernie Brandts.
Baraka alisema pia kuwa, uongozi wa Yanga umemtumia salamu za pongezi, beki Kelvin Yondani kwa kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, kinachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji, iliyoanza jana nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment