WAJUMBE wawili kati ya watatu walioteuliwa kuunda Bodi ya Yanga, wameamua kujiweka pembeni kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa klabu hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, wajumbe hao hawajalipwa mishahara yao tangu walipoteuliwa kushika nyadhifa hizo miezi mitatu iliyopita.
Wajumbe hao, Patrick Naggi kutoka Kenya na Peter Simba, wamekaririwa wakisema kuwa, wameona ni vigumu kwao kuendelea kufanyakazi Yanga wakiwa katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, tayari Naggi amesharejea kwao Kenya wakati Simba ameamua kufanya shughuli zingine nje ya zile za Yanga.
Mmoja wa watu wa karibu na Naggi, aliieleza Burudani wiki hii kuwa, Mkenya huyo alikuwa akiishi hotelini kwa muda wote aliokuwepo nchini na pia kutumia gari la kukodi.
"Kilichomshtua ni kuona kuwa, huduma zote hizo hadi sasa hazijalipwa na uongozi wa Yanga na hivyo kujikuta akiwa kwenye matatizo,"kilisema chanzo cha habari.
Kiliongeza kuwa, Naggi alirejea kwao Kenya baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara na alilazimika kukopa fedha za nauli.
Mkenya huyo aliletwa nchini kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako.
Chanzo chetu cha habari kieleza kuwa, kuondoka kwa Naggi ni ishara kwamba, hatarajii kurudi tena nchini na ameshaanza kutafuta kazi sehemu nyingine.
Katika hatua nyingine, imebainika kuwa watendaji kadhaa wa klabu ya Yanga hawana mikataba na wamekuwa wakifanyakazi kienyeji.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, miongoni mwa wasiokuwa na mikataba ni pamoja na Kocha Msaidizi, Fred Felix Minziro na maofisa wenzake wa benchi la ufundi, akiwemo daktari.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Minziro amekuwa akipigwa danadana kila anapoomba kupatiwa mkataba na hali hiyo imewafanya yeye na wenzake kuwa na hofu ya kupoteza haki zao iwapo utakuja uongozi mpya.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo jana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kaziguto alisema hawezi kuyatolea majibu kwa vile hajapata taarifa hizo kutoka kwa viongozi.
No comments:
Post a Comment