KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 3, 2013

TUTAZIFUNGIA TIMU KUCHEZA NA MASHABIKI-MALINZI




Ndugu Leodegar Tenga Rais aliyemaliza muda wake

Ndugu Said El Maamry Mwenyekiti mstaafu wa iliyokuwa FAT

Ndugu Muhidin Ndolanga Mwenyekiti mstaafu wa

iliyokuwa FAT

Wajumbe wa Baraza la Wadhamini

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji

Wafanyakazi wa TFF

Wageni waalikwa

Mabibi na Mabwana

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hapa leo.

Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kukupongeza Rais wetu uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar Tenga na Kamati yako ya utendaji . Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa, historia haitawasahau. Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi inayoheshimika ndani na nje ya mipaka ya nchi hii, nawashukuru na kuwapongeza sana.

Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa mrefu. Wapo walioshinda na wapo ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna kazi moja tu kujenga mpira. Kama tulikwaruzana kwenye kampeni tusameheane, tuwe kitu kimoja, tuinyanyue soka yetu. Makundi hayajengi yanabomoa, tuachane nayo.

Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia madarakani alfajiri ya tarehe 28-11-2013 unakabiliwa na changamoto nyingi. Nitaelezea changamoto chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

1. Mashindano yanayotukabili.

Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali ya kimataifa. Mfano ni mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji wiki ijayo, Mitoano ya mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano ya Chalenji Novemba mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote haya yanahitaji maandalizi ya haraka.



2. Programu ya vijana.

Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea azma ya Tanzania kuomba uenyeji wa fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019. Jambo hili tutalizungumzia kwenye kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na timu nzuri ya kucheza fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho kuunda timu ya Taifa ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya vijana tutakayoiandaa sharti ijielekeze kwenye ratiba hii.



3. Udhamini wa timu za vijana na za wanawake

Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF. Timu zetu za Taifa kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni brands inabidi ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa hizo timu. Kitengo cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto hizi. Mdhamini ni mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani anategemea matokeo mazuri kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende kwa wadhamini tuwashawishi waone watafaidikia nini (leverage) kwa kudhamini timu zetu. Tusisubiri waje tuwafuate sisi.


4. Uwekezaji

Jitihada za haraka lazima zifanyike kuiongezea TFF uwezo wa kiuchumi. Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant) atafutwe atufanyie mchanganuo wa uwekezaji katika ardhi yetu hii ya Karume ili tuwekeze kitega uchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa zenye nembo yetu zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki yake.

Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee suala la fujo viwanjani. Mpira ni dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa mwamuzi unakuwa ni wa mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha nyuma ya kivuli cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya makusudi au ya bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio mashabiki. Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya mechi ya mpira kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za FIFA, CAF na TFF ziko wazi na adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi ni timu husika kucheza kwenye uwanja mtupu usio na mashabiki kama ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri au kucheza nje ya uwanja wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu Dakar, Senegal waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na wakachagua kuchezea Morocco.

Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na Dar es salaam wote tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema iwe mara ya kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya kanuni uongozi wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye ligi yetu. Ni jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao. Tabia ya benchi la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za mashabiki ni kinyume na taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili. Viongozi wa klabu na mabenchi yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza wajibu wao tusilaumiane.

Ndugu zangu ya kufanya ni mengi katika kuiendeleza soka yetu. Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi tunao na tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira. Ombi langu kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote kuanzia Serikali, Halmashauri, mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina imani tukishikamana tutaifikia ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira kwenye anga za dunia.

Ahsanteni nawashukuru sana.

No comments:

Post a Comment