KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 21, 2013

RAGE: WANANIOGOPA



SIKU moja baada ya Kamati ya Utendaji ya klabu ya Simba, kumsimamisha Mwenyekiti wake, Ismail Rage, mwenyekiti huyo amesema hautambui uamuzi huo.

Katika taarifa yake, aliyoitoa jana kwa njia ya mtandao, Rage alisema
kamati ya utendaji haina mamlaka ya kumsimamisha kwa kuwa haikufuta utaratibu.

Rage alisema tuhuma na uamuzi uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo, hauna mashiko na kuongeza kuwa, atazungumzia suala hilo kwa kina baada ya kurejea nchini kesho akitokea Sudan.

Aliongeza kuwa, iwapo kamati ya utendaji ya Simba haikuwa na imani naye kama ilivyodai, ilipaswa kumjadili katika vikao vingine vilivyofanyika akiwa hapa nchini..

Rage alisema anashangaa kuona kamati hiyo imepitisha uamuzi huo wakati akiwa hayupo nchini na kuhoji kwanini isitoe uamuzi huo akiwa ndani ya kikao hicho.

"Awali, wanachama wapatao 700 walitangaza kunipindua na wakatoa sababu lukuki, lakini sikuondoka, hivyo hata uamuzi wa sasa wa kamati hiyo hauna maana, wanahitaji kujipanga upya," alisema Rage.

Alisema anasubiri kupata barua ya uamuzi huo kutoka kwa kamati hiyo kabla ya kuzungumza na kujua hatma ya uamuzi huo, ambao amesisitiza kuwa, hawezi kuutambua.

Kamati ya Utendaji ya Simba, chini ya Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang'are 'Kinesi', ilitangaza kumsimamisha Rage kutokana na kukosa imani naye huku ikiwatupia virago Kocha Mkuu, Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo 'Julio'

Kinesi aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa, uamuzi wa kumsimamisha Rage una lengo la kuboresha utendaji kazi ndani ya klabu hiyo kutokana na Rage kutoa maamuzi binafsi bila kuwashirikisha viongozi wenzake.

Alisema moja ya makubaliano aliyokiuka Rage ni kusimamisha mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba, uliopangwa kufanyika mwezi huu huku akiyaagiza matawi kuendelea kutuma taarifa ya marekebisho ya katiba hiyo.

Alizitaja tuhuma zingine zilizosababisha Rage asimamishwe uongozi kuwa ni kuingia mkataba na Azam TV bila makubaliano na viongozi wenzake na kumuuza mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile Sahel ya Tunisia bila Simba kulipwa fedha.

Wakati huo huo, siku moja baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba kumng'oa mwenyekiti wao, Ismail Rage kwa madai ya kukosa imani naye, klabu hiyo imewasilisha taarifa rasmi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusu uamuzi huo.

Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura, alisema barua hiyo waliipokea jana na itafikishwa kwenye kamati husika kwa kupitiwa kisha kutolewa uamuzi.

Kwa sasa TFF haina kamati hata moja baada ya kuvunjwa na Rais mpya, Jamal Malinzi, ambaye aliahidi kuunda zingine baada ya kuanza kazi kwenye taasisi hiyo.

Hata hivyo, Wambura aliahidi taarifa hizo za Simba zitajadiliwa na kamati husika ndani ya kipindi kifupi na kutolewa uamuzi kuhusu taratibu za kisheria zilizotumika 'kubariki' mapinduzi hayo ndani ya klabu hiyo.

"Si kwamba taarifa hizo tumesoma au kusikia kwenye vyombo vya habari bali, tunazo rasmi kwani tumeletewa barua inayoeleza kuhusu kusimamishwa Mwenyekiti wa Simba," alisema Wambura.

Katibu huyo alisema, binafsi hawezi kutoa ufafanuzi wowote kuhusu kilichofanywa na kamati ya utendaji ya Simba kwa kuwa kinyume na taratibu za utendaji za shirikisho hilo.

"Ni suala la kamati, ambazo zinafanya kazi kwa niaba ya kamati ya utendaji ya TFF," alifafanua Wambura.

Hatima ya Rage iko mikononi mwa Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji za kurudishwa madarakani au kupigwa chini rasmi baada ya kuketi kujadili sakata hilo jipya katika klabu hiyo.

Mwenyekiti huyo kama atarudishwa madarakani itakuwa mara ya pili kuwashinda 'wana mapinduzi', kwani mapema mwaka huu wanachama wa Simba wapatao 700 waliokutana kwenye Hoteli ya Star Light jijini, Dar es Salaam, walimwengua katika uongozi na kupeleka taarifa hiyo TFF, lakini waligonga mwamba.

No comments:

Post a Comment