KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 28, 2013

USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema usajili wa dirisha dogo, ulioanza mapema mwezi huu, unatarajiwa kufungwa Desemba 15 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na TFF kwa vyombo vya habari juzi, imezitaka klabu zote zinazoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, kuheshimu kanuni na kuzingatia muda uliowekwa.
"Pia tunapenda kuzikumbusha klabu kuwa, kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine, hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30, maana yake ni kwamba, haina nafasi ya kuongeza wachezaji," imesema taarifa hiyo.
 TFF imesema, kwa upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), kuanzia msimu ujao wa 2014/2015, watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Imesema pia kuwa, kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje, mpaka sasa hakuna hata klabu moja iliyoingia kwenye TMS kuomba uhamisho.
"Itakapofika Desemba 15, utaratibu huo wa TMS utafungwa," imesema taarifa hiyo.
Wakati huo huo, TFF imesema, imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, alisema juzi kuwa, Kiloyi alifariki dunia Novemba 24 mwaka huu kutokana na ugonjwa wa fangasi ya ubongo.
Kwa mujibu wa Mahano, mwili wa marehemu Kiloyi umesafirishwa kwenda kwao Kigoma kwa ajili ya mazishi.
Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988, ambapo alipata beji ya FIFA mwaka 2001, akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009 na hadi anafariki, alikuwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).

No comments:

Post a Comment