KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 6, 2013

SIMBA YAIUA ASHANTI, MESSI ANATISHA, TAMBWE AFIKISHA MABAO 10


SIMBA imemaliza duru la kwanza la ligi kuu Tanzania Bara msimu huu kwa kuifanyia mauaji ya mabao 4-2 timu ya Ashanti United katika mechi iliyokuwa na presha kali.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, jana, pia ilishuhudiwa kipa wa Ashanti wa Ashanti United Amaan Simba akitolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani kwa kosa la kudaka mpira nje ya kisanduku cha hatari.

Golikipa huyo alijitoa muhanga kudaka mpira huo kutokana na beki wake kutokwa na William Lucian na hivyo kulazimika kujitosa kuokoa jahazi bila mafanikio kwa sababu mpira huo ulikuwa mrefu kwake.

Awali mechi hiyo ilianza kwa kukamiana na Ashanti ilibisha hodi langoni mwa Simba katika dakika ya nne, lakini Joseph Mahundi alishindwa kuunganisha wavuni mpira wa adhabu ilitokana na Paul Maona kuchezewa madhambi.

Simba walijibu mapigo dakika moja baadaye kupitia kwa kiungo Amri Kiemba aliyewalamba chenga mabeki wa Ashanti na kupiga krosi iliyotua kichwani kwa Amis Tambwe, lakini mpira huo ulipaa kwenye lango la Ashanti.

Mshambuliaji machachari Ramadhani Singano 'Messi' aliwatoka mabeki wa Ashanti na kufumua shuti ambalo lilimpita kipa Amaan Simba na kujaa wavuni katika dakika ya nane.

Idd Said wa Ashanti alionywa kwa kadi ya njano baada ya kumchezea faulo Tambwe katika dakika ya 21, adhabu iliyotolewa pia kwa Jonas Mkude aliyemkwatua Mahundi.

Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya 1-1 kufuatia Hussein Sued kusawazisha kwa kichwa katika dakika ya 45 akijitwisha krosi murua ya Said Maulid 'SMG' aliyeichachafya vikali ngome ya Simba katika kipindi hicho.

Kipindi cha pili ilikuwa zamu ya mashabiki na benchi la ufundi la Simba kucheka na kushusha presha, baada ya kuanza mchezo kwa kasi na kufunga mabao kama 'mvua'.

Tambwe mshambuliaji kutoka Burundi alizidi kujichimbia katika usukani wa washambuliaji wanaoongoza kwa ufungaji katika ligi kuu ya bara msimu huu, kwa kufunga bao la pili la Simba katika dakika ya 46.

Mrundi huyo alisindikiza mpira wavuni kwa pasi ya Singano aliyekuwa nyota wa mchezo huo kutokana na kuonyesha ufundi wa kuipangua ngome ya wauza mitumba wa Ashanti.

Hakuna lugha fasaha ya kueleza zaidi ya kusema jana ilikuwa siku ya Singano aliyefanya kazi nyingine nzuri ya kuichambua ngome ya Ashanti na kutoa pasi kwa Mwombeki aliyefunga bao la tatu kiulaini katika dakika ya 49.

Mshambuliaji mkongwe nchini SMG aliwarudisha Ashanti katika hali ya mchezo kwa kufunga bao la pili kwa shuti kali akiunganisha nyavuni mpira wa krosi ya juu, lakini hali ilizidi kuwa ngumu kwao baada ya Mwombeki kuwatandika bao la nne kwa kichwa katika dakika ya 69.

Pasi iliyozaa bao la Mwombeki aliyetoka kuonyeshwa kadi ya njano dakika kabla ya kufunga bao hilo, ilipigwa na beki Haruna Shamte aliyepanda kusaidia mashambulizi ya Simba.

ASHANTI UNITED: Amaan Simba, Hussein Mkongo, Jaffar Gonga, Tumba Sued, Samir Ruhava, Idd Said/Emmanuel Memba, Fakihi Hakija, Paul Maona, Hussein Sued, Said Maulid 'SMG' na Joseph Mahundi.

SIMBA: Abuu Hashim, Haruna Shamte, Issa Rashid, Gilbert Kaze, Hassan Khatib/Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Henry Joseph/ Said Ndemla, Betram Mwombeki, Amis Tambwe na Amri Kiemba/ William Lucian.

No comments:

Post a Comment