KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 28, 2013

YANGA YAITESA ASHANTI KOMBE LA UHAI



TIMU ya soka ya vijana wa chini ya umri wa miaka 20 ya Yanga, jana ilitoa kichapo cha mabao 2-1 kwa Ashanti United, katika mechi ya michuano ya Kombe la Uhai.
Katika mechi hiyo ya robo fainali, iliyochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Mbagala, Dar es Salaam, timu zote mbili zilionyesha kandanda ya kuvutia na kuwapa burudani murua mashabiki.
Iliwachukua Ashanti dakika 32 kuhesabu bao la kwanza, lililofungwa na Juma Ally, baada ya kuwachambua mabeki wa Ashanti na kubaki ana kwa ana na kipa wa timu hiyo.
Baada ya kufungwa bao hilo, Yanga ilichachamaa na kusukuma mashambulizi mfululizo kwenye lango la Ashanti. Mashambulizi hayo yalizaa matunda dakika ya 42 baada ya Haruna Rashid kuisawazishia.
Timu zote mbili, zilikianza kipindi cha pili kwa kasi kila moja ikipania kuongeza bao la pili. Juhudi hizo zilizaa matunda kwa Yanga, iliyopata bao la pili dakika ya 75 kupitia kwa Baraka Ally.
Baada ya kufunga bao hilo, Yanga ilianza kucheza mchezo wa kujihami huku Ashanti ikihaha kusaka bao la kusawazisha, lakini milango ilikuwa migumu.
Katika mechi nyingine ya robo fainali iliyochezwa jana, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons.

No comments:

Post a Comment