KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 21, 2013

FULANA ZA MICHEZO ZAGEUZWA DILI DAR, ZINAONGOZA KWA KUUZWA NA KUVALIWA



KUANZIA mwanzoni mwa miaka ya 2000, biashara ya vifaa vya michezo imekuwa ikishamiri sana hapa nchini. Karibu sehemu kubwa ya maduka ya nguo yaliyotapakaa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, biashara yake kubwa ni kuuza vifaa vya michezo.

Vifaa vinavyouzwa kwa wingi kwenye maduka hayo ni seti za jezi, fulana, bukta, suti za michezo, mipira, soksi, raba na viatu vya kuchezea michezo ya aina mbalimbali.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Burudani kwa wiki kadhaa, vifaa vyenye nembo za klabu za Simba na Yanga, ndivyo vinavyoongoza kwa kuuzwa kwa wingi kwenye maduka hayo ya vifaa vya michezo. Vifaa hivyo ni jezi, bukta, suti za michezo, soksi, kofia na skafu.

Kwa klabu za Ulaya, vifaa vinavyouzwa kwa wingi ni vya klabu za Barcelona na Real Madrid za Hispania, Manchester United, Arsenal, Chelsea, Liverpool, Sunderland na Manchester City za England, Inter Milan, AC Milan na Juventus za Italia.

Vifaa vingine vya michezo vinavyoongoza kwa kuuzwa kwa wingi ni jezi na suti za michezo za timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jezi za Brazil, Hispania, Cameroon, Nigeria, England na Hispania.

Ukitembelea sehemu mbalimbali za kazi, burudani na michezo, ni jambo la kawaida kumuona mtu mmoja ama kikundi cha watu, wakiwa wamevaa jezi ama fulana zenye nembo za klabu mbalimbali maarufu duniani, hasa Simba na Yanga.

Hata waheshimiwa wabunge, mawaziri, viongozi wa vyama vya siasa na watumishi wa serikali ni miongoni mwa watu wanaopenda kuvaa mavazi hayo, hasa wanapokuwa kwenye michezo, matamasha ya muziki ama kwenye shughuli zingine za baada ya kazi.

Mavazi hayo hushamiri zaidi siku timu kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zinapokutana katika mechi za ligi ama zinapocheza dhidi ya timu nyingine na pia siku Taifa Stars, inapocheza mechi za kirafiki ama za kimataifa dhidi ya timu kutoka nje.

Katika siku za hivi karibuni, wamiliki wa baa nao wameyageuza mavazi hayo ya michezo kuwa sare za wahudumu wao. Mara nyingi zare hizo hununuliwa na wahudumu wenyewe kwa maelekezo ya mmiliki wa baa. Sare zinazopendwa zaidi na wahudumu ni fulana zenye nembo za Yanga na Arsenal.

Si kwamba wahudumu hao wanapenda kuvaa sare hizo kwa sababu ni mashabiki wa klabu hizo, la hasha. Ni kwa sababu ya rangi zake na uzuri wake. Ubora na kiwango cha fulana za Yanga na Arsenal kipo juu ikilinganishwa na fulana zingine.

Wakizungumzia kupendwa kwa sare hizo za michezo, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamesema, kumetokana na ushabiki wa soka.

"Watu wanapenda kuvaa jezi za klabu mbalimbali kwa sababu ya ushabiki. Kwa mfano, mimi huwezi kunivisha fulana zenye nembo ya Manchester United ama Simba kwa sababu sio shabiki wa timu hizo," amesema Jumanne Gude, mkazi wa Buguruni, Dar es Salaam.

Issaya Katembo, mkazi wa Temeke-Mwembe Yanga, Dar es Salaam, anasema huwa anaona fahari kuvaa fulana yenye nembo ya Yanga kwa sababu ndiyo klabu anayoipenda na kuishabikia.

Kwa upande wake, Jamila Hassan, mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam, anasema watu wengi wanapenda kuvaa fulana za michezo kwa sababu bei zake ni nafuu, ikilinganishwa na mashati ama fulana za kawaida.

"Kusema kweli, bei ya fulana za michezo ipo chini. Tatizo pekee ni kwamba, viwango vyake vinatofautiana. Zipo fulana za kiwango cha juu, cha kati na cha chini. Na hata bei zake zinatofautiana kwa sababu ya ubora," amesema Jamila.

Abbas Jamal, mkazi wa mtaa wa Mkunguni, Dar es Salaam amesema, anapenda zaidi kuvaa fulana za michezo badala ya mashati, kwa sababu zinafiti kwa suruali ya aina yoyote, hasa jeans.

Muhudumu wa baa ya Kisauni iliyoko Kiwalani, Dar es Salaam, Frida Kessy anasema, alipoanza kazi, alikuta wenzake wakiwa wanavaa fulana zenye nembo ya Yanga na Arsenal, hivyo naye hakuwa na budi kufanya hivyo.

"Mimi sio shabiki wa Yanga wala Arsenal, nalazimika kuvaa fulana hizi kwa sababu ndiyo sare ya wafanyakazi na tunalazimika kujinunulia wenyewe,"amesema.

Mkurugenzi wa Masoko wa duka la vifaa vya michezo la Isere Sports, lililoko mtaa wa Mchikichi, Dar es Salaam, Abbas Isere amekiri kuwa, biashara hiyo kwa sasa inalipa kutokana na kumwingizia fedha nyingi.

Abbas amesema katika duka lake hilo, amekuwa akiuza fulana za michezo zenye nembo za klabu mbalimbali maarufu duniani, lakini anazouza zaidi ni za timu za Barcelona, Real Madrid, Manchester United, Chelsea na Liverpool.

"Vifaa vyangu vyote ninavyouza hapa dukani ni orijino na vya kiwango cha juu ndio sababu bei zake zipo juu kidogo. Siuzi vifaa feki. Nauza vifaa orijino kwa lengo la kuimarisha biashara yangu na ninaviuza kwa bei ya jumla na rejareja," amesema Abbas.

Mkurugenzi huyo amesema pia kuwa, fulana za Simba na Yanga na zile zenye nembo na rangi ya Taifa Stars, ndizo zinazoongoza kwa mauzo, hasa timu hizo zinapofanya vizuri katika michuano ya ligi na kimataifa.

Ameongeza kuwa, amekuwa akiuza jezi kwa bei ya sh. 500,000 kwa seti moja na kuongeza kuwa, bei ya fulana ni kati ya sh. 20,000 na sh. 15,000 kwa kutegemea ubora wake.

"Kwa sasa nataka nifungue duka lingine la vifaa vya michezo Dodoma baada ya kupokea maombi kutoka kwa baadhi ya wabunge. Natarajia kufanya hivyo hivi karibuni,"amesema Abbas.

No comments:

Post a Comment