KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 17, 2010

YANGA ARUSHA WAMPA TUZO MBUNA


UONGOZI wa tawi la klabu ya Yanga la mjini Arusha umempa tuzo maalumu mchezaji Fred Mbuna kutokana na kudumu kwenye timu hiyo kwa miaka kumi.
Mbali na tuzo hizo, ambazo ni cheti na ngao, tawi hilo pia limemzawadia mchezaji huyo pesa taslimu sh. 300,000.
Mbuna alikabidhiwa tuzo hizo na Mwenyekiti wa Yanga tawi la Arusha, Haji Haji wakati wa mechi ya ligi kuu ya soka ya Vodacom kati ya timu hiyo na AFC iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Beki huyo aliyesajiliwa na Yanga mwaka 2000 akitokea Majimaji ya Songea, alikabidhiwa tuzo hizo wakati wa mapumziko, mbele ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyord Nchunga na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Isidore Shirima.
Katibu Mipango wa tawi hilo, Angelo Mweleka alisema wameamua kumzawadia Mbuna tuzo hizo kutokana na kuthamini mchango wake kwa timu ya Yanga.
“Mbuna ni mchezaji pekee wa Yanga aliyedumu kwenye klabu hiyo kwa miaka kumi bila kutoka na ametoa mchango mkubwa kwa Yanga na ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wengine,”alisema.
Mweleka alisema tawi lao kwa kushirikiana na uongozi wa Yanga, wanafanya mipango ili mchezaji huyo apatiwe nafasi ya kusomea ukocha baada ya kustaafu soka.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Mbuna aliishukuru uongozi wa Yanga tawi la Arusha na kuzitaka klabu zingine ziige mfano huo.
Mbuna alisema binafsi hakutarajia kupewa tuzo hizo na kuwataka wachezaji wengine wa Tanzania kuiga mfano wake kwa kudumu kwenye klabu zao kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment