KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 1, 2010

Robinho atua AC Milan, Asamoah atinga Sunderland


LONDON, England
KLABU kadhaa za ligi kuu za Ulaya juzi zilikamilisha usajili wa wachezaji wake wapya kwa ajili ya msimu wa ligi wa 2010-2011.
Katika usajili huo, klabu ya AC Milan ya Italia ilifanikiwa kumnyakua mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Robinho de Souza kutoka klabu ya Manchester City ya England.
Kabla ya kusajiliwa na AC Milan, Robinho aliichezea kwa mkopo klabu yake ya zamani ya Santos ya Brazil.
Wachezaji kadhaa nyota waliong’ara katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini nao walitumia nafasi hiyo kujiunga na klabu zingine, akiwemo mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Asamoah Gyan aliyejiunga na Sunderland ya England akitokea Rennes ya Ufaransa.
Katika usajili huo, kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Rafael van der Vaart amejiunga na klabu ya Tottenham ya England akitokea Real Madrid ya Hispania wakati Klaas-Jan Huntelaar, Jose Manuel Jurado na beki Nicolas Plestan wamejiunga na Schalke ya Ujerumani.
Klabu za Barcelona, Real Madrid, Inter Milan, Manchester United na Chelsea hazikufanya usajili wowote wa kutisha katika dakika za mwisho baada ya kukamilisha usajili wa awali wiki kadhaa zilizopita.
Usajili wa wachezaji wa ligi kuu ya England msimu huu haukuwa mkubwa ikilinganishwa na msimu wa 2009. Pauni milioni 100 za Uingereza zinakadiriwa kutumika katika usajili wa msimu huu.
Klabu pekee iliyoripotiwa kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji wapya msimu huu ni Manchester City. Klabu hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara Sheikh Mansour kutoka Arabuni, inakadiriwa kutumia zaidi ya pauni milioni 300 za Uingereza.
Miaka miwili iliyopita, Manchester City iliishtua dunia baada ya kumsajili dakika za mwisho mshambuliaji Robinho akitokea Real Madrid. Usajili wa mshambuliaji huyo uliigharimu Manchester City pauni milioni 32. ikiwa ni rekodi kwa klabu za England.
Hata hivyo, Robinho alishindwa kuonyesha cheche zake katika ligi hiyo, hatua iliyosababisha Manchester City imuuze kwa mkopo kwa klabu yake ya zamani ya Santos.
AC Milan imeripotiwa kutumia pauni milioni 15 kumsajili Robinho kwa mkataba wa miaka minne. Mbrazil huyo atalazimika kupigania namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo chenye wachezaji wengine nyota kama vile Zlatan Ibrahimovic, Ronaldinho Gaucho na Alexander Pato.
Lengo la AC Milan kufanya usajili kabambe msimu huu ni kumaliza ukame wa miaka mitano wa kushindwa kushinda taji la ligi ya Serie A ya Italia. Taji hilo limekuwa likinyakuliwa mara kwa mara na mahasimu wao Inter Milan.
Kuwasili kwa Robinho kwenye klabu hiyo kulitoa nafasi kwa mshambuliaji, Huntelaar kuhamia Schalke ya Ujerumani kwa mkataba wa miaka mitatu.
“Lengo letu linapaswa kuwa ni kushinda kila taji,” alisema Robinho baada ya kumwaga wino AC Milan. “Wabrazil wote kwenye timu watanipa sapoti kwenye kikosi. Natarajia kuweka historia kwa klabu.”
Kocha Mkuu wa Schalke, Felix Magath, ambaye amewatema wachezaji kadhaa wakongwe, amemuongeza kwenye kikosi chake Plestan kutoka Lille ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu na kiungo Jurado kutoka Atletico Madrid kwa mkataba wa miaka minne.
Birmingham ya England nayo ilifanya usajili wa wachezaji watatu kwa mipigo dakika za mwisho, akiwemo kiungo Alexander Hleb kutoka Barcelona, kiungo Jean Beausejour kutoka Club America ya Mexico na beki Martin Jiranek kutoka Spartak Moscow ya Russia.
Sunderland iliweka rekodi mpya ya usajili baada ya kumnyakua mshambuliaji Fraizer Campbell. Kabla ya usajili huyo Campbell alikuwa majeruhi kwa miezi sita.
Kadhalika, mmiliki wa klabu hiyo Ellis Short amelipa zaidi ya pauni milioni 13 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji Gyan, ambaye mabao yake yaliisaidia Ghana kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu.
Mshambuliaji Eidur Gudjohnsen wa Monaco amerejea tena katika ligi kuu ya England, lakini safari hii amejiunga na klabu ya Stoke City kwa mkopo wa muda mrefu. Klabu hiyo pia imemsajili Jermaine Pennant kwa mkataba wa miezi sita akitokea Real Zaragoza ya Hispania.
Liverpool ndiyo klabu pekee kongwe ya England iliyofanya usajili dakika za mwisho baada ya kumnasa beki Paul Konchesky kutoka Fulham. Beki huyo ametia saini mkataba wa miaka minne.
Konchesky amesajiliwa ili kuziba pengo la beki chipukizi wa Argentina, Emiliano Insua, aliyeihama Liverpool na kujiunga na klabu ya Galatasaray ya Uturuki.
Joseph Yobo wa Everton ameihama klabu hiyo na kujiunga na Fenerbahce ya Uturuki wakati Armand Traore wa Arsenal ametua rasmi Juventus ya Italia.
Usajili uliosisimua katika ligi kuu ya Hispania ni wa mchezaji David Trezeguet, aliyejiunga na klabu mpya katika ligi hiyo, Hercules kwa mkataba wa miaka miwili. Trezeguet aliichezea Juventus ya Italia kwa misimu 10.
Nayo Valencia imefanikiwa kumsajili kwa mkopo mshambuliaji Marius Stankevicius kutoka Sampdoria ya Italia ilu kuziba pengo la mabeki Carlos Marchena na Alexis Ruano, waliouzwa kwa Sevilla wiki iliyopita.
Klabu ya Bordeaux ya Ufaransa nayo imemsajili kiungo Abdou Traore kutoka Nice, akiwa ni mchezaji wa pili baada ya kusajiliwa kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Serbia, Danijel Ljuboja kutoka Grenoble.

No comments:

Post a Comment