KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 2, 2010

MR. NICE: Maadui zangu ndio walionifikisha nilipo


Akanusha madai kuwa amefilisika na kufulia
Albamu yake mpya ya ‘Wakinuna’ ipo sokoni

MSANII machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Lucas Nkenda, maarufu kwa jina la Mr. Nice amesema maadui zake ndio waliofikisha alipo sasa kimuziki.
Akihojiwa katika kipindi cha Mamboyoyo kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha ITV mwishoni mwa wiki iliyopita, Mr. Nice alisema amefanikiwa kupanda tena chati kimuziki kutokana na kuwa maadui wengi.
Mr. Nice alisema bila kuwa na maadui, si rahisi kwa msanii ama mtu mwingine yeyote kupata mafanikio katika maisha yake kwa sababu ni wao ndio wanaompa nguvu ya kufanya ayafanyayo.
“Kuna rafiki yangu mmoja wa karibu sana aliwahi kuniambia, ‘siku zote anayefanya mazuri huandamwa na mambo mengi katika maisha yake’. Nami sasa nimeamini, usipokuwa na maadui wengi huwezi kufanikiwa. Maadui zangu ndio walionifikisha hapa nilipo,”alisema msanii huyo.
Msanii huyo, ambaye amekumbwa na misukosuko mingi kimaisha, alisema ameifanyia mambo mengi makubwa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuitangaza kimataifa.
Alisema katika maisha yake kimuziki, ameshafanya maonyesho zaidi ya 28 katika sehemu mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na kubuni aina yake ya muziki, ambayo imeigwa na wanamuziki wengi, ndani na nje ya Tanzania.
Mr. Nice alisema japokuwa kwa sasa amesahaulika kimuziki huku baadhi ya watu wakidai kuwa, amefilisika kimuziki, ipo siku ukweli utabainika na itajulikana umuhimu wake kimuziki.
Katika kudhihirisha hilo, Mr. Nice alisema kwa sasa anajiandaa kupakua albamu yake mpya, itakayojulikana kwa jina la ‘Wakinuna’. Alisema albamu hiyo itakuwa na vibao vinane alivyovipiga katika miondoko tofauti.
“Albamu yangu mpya itakuja na vitu tofauti, itadhihirisha kwamba ukimya wangu haukuwa wa bure,” alisema msanii huyo.
Mr Nice alisema amerekodi nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo kupitia kampuni yake binafsi, inayojulikana kwa jina la Bushclick na pia kufanyakazi ya kuisambaza yeye mwenyewe ili kupambana na tatizo la wizi wa kazi za wasanii.
“Nimeamua kuyafanya yote hayo ili hata kama itakuwa haina ubora, lawama zote zije kwangu,”alisema.
Msanii huyo mwenye makeke awapo stejini alisema vibao vyake vingi vilivyomo kwenye albamu yake mpya, vinaweza kuonekana kama vile vinazungumzia masuala ya mapenzi, lakini ndani yake kuna ujumbe mzito.
“Kuna vijembe vya hatari, kuna mambo ya mapenzi, siasa, chuki na bila kuwasahau watoto wadogo, ambao ndio kanisa langu na mhimili wangu mkubwa,”alisema.
Msanii huyo aliyejizolea umaarufu mkubwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati alisema anawashukuru watu mbalimbali waliompa moyo baada ya kuonekana amefilisika kimuziki.Alisema watu hao ndio waliomwezesha kujipanga upya ili aweze kutoka kivingine.
Amekanusha katakata madai kuwa amefilisika kimuziki na kuongeza kuwa, ukimya wake ni ishara kwamba alikuwa akijipanga upya ili kutoka na staili nyingine tofauti.
“Huwezi kusema kuwa nimefulia kimuziki ama kifedha wakati aina ya muziki wangu hakuna mtu anayeweza kuiga wala kuifanya. Bado niko mwenyewe na matoleo niliyoyatoa bado yanafanya vizuri sokoni,”alisema.
“Kama kukaa kimya bila kutoa albamu mpya au kupanda jukwaani ama kutoonyesha uwezo wako kifedha ndiyo maana ya kufulia, basi mimi sijafulia tena niko juu zaidi,” aliongeza.
“Kuna watu waliofulia tunawafahamu na hatuwezi kuwasema. Walianza muziki kwa mbwembwe na baadaye wakakwama ghafla na hii ilitokana na kubebwabebwa tu na baadhi ya watu kwa sababu ya faida za wachache, lakini sio kweli kwamba wana uwezo mkubwa kisanaa.
“Baada ya kutoa singo zao ama albamu zao za kuungaunga, wakajiona masikio yanazidi kichwa na walipoachwa ili waonyeshe uwezo wao wenyewe, wakashindwa. Hao ndiyo waliofulia, sio mimi bwana mi niko juu sana,”alisema msanii huyo.
“Mimi muziki kwangu ni kazi na ndiyo ajira yangu hivyo ni lazima niwe na malengo makubwa ili ninufaike katika maisha yangu yote kwa sababu nimebaini kuwa ni kazi pekee inayonifaa na kunipa mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi,” aliongeza.
Mr. Nice alijizolea umaarufu mkubwa alipoibuka na vibao vyake vilivyotamba kama vile ‘Kidali po’, ‘Kila mtu na demu wake’, ‘Kikulacho’, ‘Fagilia’, ‘Mbona umeniacha’, ‘Rafiki’ na ‘First Lady’.

No comments:

Post a Comment