KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, September 17, 2010

ALI MUSTAFA BARTHEZ


UNAPOWAZUNGUMZIA wachezaji tegemeo kwa sasa ndani ya kikosi cha Simba, ni vigumu kuacha kulitaja jina la kipa Ali Mustapha 'Barthez', aliyeanza kujizolea sifa baada ya kuumia mkono kwa kipa namba moja Juma Kaseja. Kipa huyo amekuwa gumzo siku za hivi karibuni baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kulinda lango la timu hiyo kwenye michezo aliyopangwa, hususan ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na mwandishi wa blogu hii, kipa huyo anaelezea mafanikio yake kisoka.

SWALI: Kipa Ali Mustapha, unaweza kueleza historia yako kwa ufupi?
JIBU: Nimezaliwa jijini Dar es Salaam mwaka 1984, wazazi wangu wanaishi Ukonga, Majumba Sita. Nilihitimu elimu ya msingi katika shule ya Karakata mwaka 2001 na sikubahatika kuendelea na elimu ya sekondari. Nilianza kucheza soka tangu nilipokuwa nasoma.
SWALI:Ulicheza katika timu zipi kabla ya kusajiliwa na Simba?
JIBU:Nimecheza timu nyingi zikiwemo Mogo FC ya Karakata, Pentagon, Mkunguni, Kumbukumbu, Ashanti United iliyokuwa Ligi Kuu na nyingine nyingi za nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
SWALI: Unakumbuka ulisajiliwa Simba mwaka gani?
JIBU:Nilijiunga na kikosi cha Simba mwaka 2005 na kuanzia hapo nilizidi kujifunza mengi kuhusu klabu hiyo na mchezo wa soka kwa ujumla.
SWALI: Nini kilikuvutia hadi kuamua kuchezea Simba badala ya timu nyingine?
JIBU:Mtu aliyenisukuma nitue Simba ni golikipa Mohamed Mwameja, ambaye alikuwa ananivutia sana enzi zake alipokuwa anadakia klabu hiyo. Sio siri huyu jamaa alinivuta sana kuichezea Simba kutokana na uwezo aliokuwa nao na mimi nimeiga baadhi ya mbinu zake.
SWALI:Mambo gani ambayo umejifunza tangu ulipojiunga na kikosi cha Simba?
JIBU:Unajua timu kama Simba ina watu wenye uelewa tofauti; kuna wasomi na wenye elimu ya kawaida ambao kila mmoja ana tabia zake. Kutokana na kuwepo hali hiyo, nimekumbana na wakati mgumu timu inapopata matokeo mabaya, lakini tunapofanikiwa kutwaa kombe lolote, kinakuwa kipindi kizuri kwetu wachezaji na wana Simba wote kwa sababu furaha inatawala kila mahali.
SWALI: Changamoto zipi umekutana nazo Simba?
JIBU:Changamoto ni kubwa kwani bila ya kujituma nisingedumu miaka hiyo na nafikiri ningekuwa nimeshaondoka siku nyingi. Naheshimu kazi inayonipa riziki ya kila siku na familia yangu na nimefika hapa kutokana na maelekezo mazuri ya makocha walionifundisha katika timu zote nilizocheza. Siwataji majina, lakini nawashukuru sana.
SWALI: Umekuwa unapambana na kipa Juma Kaseja kusaka namba katika kikosi cha kwanza cha Simba, unazungumziaje ushindani huo?
JIBU:Mchuano upo kati yetu, lakini sio siri napenda kumpongeza Kaseja, amekuwa ananipa changamoto kubwa ya kuongeza juhudi katika mazoezi na tunashirikiana vizuri.Bado kuna kazi kubwa ya kufikia malengo. La muhimu ni kujituma kwenye mazoezi na kuwa makini kwa mambo mengine ya nje ya uwanja na kuzingatia masharti ya vyakula na afya.
SWALI: Kukosekana Kaseja baada ya kuumia kidole kumekupa mwanya wa kuonyesha uwezo wako, je unajisikiaje?
JIBU:Binafsi nimesikitika Kaseja kuumia, lakini nimepata muda wa kuonyesha uwezo wangu.Nilikuwa najifua kwa nguvu ili niweze kufanya vitu vyangu kwenye michezo hiyo, ukiwemo dhidi ya Yanga wa kuwania Ngao ya Hisani.
Licha ya mchezo huo, ambao tulipoteza kwa bahati mbaya, nimeweza kuonyesha uwezo wangu katika mechi ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya na Azam, ambayo ilikuwa ya Ligi Kuu iliyochezwa wiki iliyopita mkoani Tanga.
SWALI: Nini siri ya mafanikio yako katika mechi hizo?
JIBU: Kwanza kabisa siri ya mafanikio yangu ni kufanya mazoezi muda mwingi na kingine ni umoja uliopo ndani ya kikosi cha Simba. Pia najitahidi kusoma mbinu mbalimbali za kuzuia mashuti langoni ili niwe katika kiwango cha juu. Miiko ya soka ni suala ambalo pia nalizingatia ninapokuwa kambini.
SWALI: Je, umeoa na una watoto wangapi?
JIBU:Nimeoa na nimebahatika kupata mtoto mmoja, ambaye anaitwa Mustapha ana umri wa mwaka mmoja na nusu. Kwa kweli nazingatia sana kutunza mwili wangu ili niendelee kudaka miaka mingi.
SWALI:Timu zipi za nje unazopenda kuziona zinapocheza uwanjani?
JIBU:Mimi ni mpenzi mkubwa wa timu ya Manchester United, ambayo kila inapocheza inavuta hisia zangu. Navutiwa na timu hiyo kwa sababu ya kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali. Napata changamoto ya kujituma ili niwe mchezaji mzuri kila mara kama walivyo wa timu ya Mashetani Wekundu.
SWALI:Kipi unapenda kuwaeleza wapenzi wa soka nchini?
JIBU:Nawaomba viongozi na wapenzi wa soka wajaribu kuwaamini wachezaji wao. Kila mtu anafahamu wazi majukumu yake. Hakuna mchezaji ambaye anaweza kuhujumu timu hata siku moja, kwani tunajua timu inapofanya vizuri tunanufaika. Viongozi watazame upya mbinu za kudhibiti mapato milangoni kwa sababu sisi ndio ajira yetu, hatuna vyanzo vingine vya mapato, wachezaji tunajisikia vibaya tunaposikia watu wamekamatwa na tiketi bandia. Wakati tunavuja jasho uwanjani, kumbe kuna wengine wananufaika kitu ambacho ni kibaya. Udhibiti wa mapato uongezwe.
Mwisho, naiomba serikali ijenge viwanja zaidi vya michezo kwa ajili ya kuongeza hamasa ya mchezo wa soka. Ikifanyika hivyo, vijana wengi wenye vipaji watajitokeza na watalisaidia taifa kupiga hatua mbele zaidi kisoka.

No comments:

Post a Comment