BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka viongozi wa bendi za muziki wa dansi nchini, kuacha mara moja tabia ya kuwadhalilisha wacheza shoo (wanenguaji) kwa kuwavalisha mavazi ya kutia aibu na yanayodhalilisha utu wao.
Mbali na kupiga marufuku uvaaji wa mavazi hayo, BASATA imewataka wanenguaji hao, kuthamini utu wao na kufikiria upya dhana kwamba bila kuvaa nusu uchi, sanaa ya muziki wa dansi haiwezi kupata soko na kuvutia watazamaji wakati wa maonyesho.
Akizungumza wakati wa semina ya Jukwaa la Sanaa, inayoandaliwa kwa pamoja na BASATA na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz),Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche Materego alisema, lazima wadau wa muziki wa dansi wafikirie upya na kubadili mara moja tabia ya kuendekeza maonyesho yanayochafua maadili ya mtanzania.
“Wanenguaji lazima wafikie hatua waseme kwamba, udhalilishaji huu wa nusu uchi basi tena.Wavae mavazi yenye heshima kama wanavyovaa wale wa kiume,” alisema.
Aliongeza kuwa, dhana kwamba bila wanenguaji kuvaa nusu uchi maonyesho ya muziki wa dansi hayapati watazamaji na biashara haifanyiki, ni ya uongo na inaonyesha jinsi wasanii wa dansi walivyokosa ubunifu wa kuvutia watu kwenye maonyesho yao, badala yake kubaki wakiendeshwa na hisia zisizo za kisanaa.
“Ushindani wa kibiashara, ambao unaomfanya msanii kuwa dhalili ili kuvuta watu kwenye maonyesho haukubaliki, bali unawafanya wasanii kuwa makapuku na wanaopoteza thamani yao,” aliongeza.
Alisisitiza kwamba, BASATA imekuwa ikikemea na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya unenguaji wa nusu uchi, lakini mabadiliko yamekuwa ni ya muda na baadaye kurudi kwenye udhalilishaji uleule.
Aliongeza kuwa kwa sasa, baraza lake linafanya utafiti kwenye sanaa ya unenguaji na mara utakapokamilika, mwongozo kwenye sanaa hii utatolewa na kutakiwa kufuatwa na wadau wote.
Kwa upande wake, mwasilishaji wa mada ya unenguaji wa nusu uchi,Nsao Shalua, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa ya BASATA alisema, mavazi katika kazi ya sanaa yapo kwa ajili ya kuwakilisha tamaduni za jamii husika, hivyo vichupi vinavyoonekana kwenye majukwaa havina utambulisho wala maana yoyote.
“Maleba (mapambo/mavazi) katika sanaa yoyote yanakuwa na utambulisho wa jamii na kazi husika, hivyo vivazi vya nusu uchi vinavyovaliwa havina nafasi,” alisema.
Katika Jukwaa hilo la sanaa, lililopambwa na maonyesho ya wanenguaji kutoka bendi mbalimbali nchini, waliokuwa katika mavazi tofauti, wadau wengi walilamika juu ya mavazi ya kutia aibu wanayovaa wanenguaji na kutoa mwito kukomeshwa mara moja.
No comments:
Post a Comment