KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 22, 2010

SIMBA: Tunahujumiwa

Na Peter Katulanda, Mwanza
SIKU chache baada ya kupata kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Polisi ya Dodoma, wachezaji wa timu ya soka ya Simba wamedai kuwa, wamekuwa wakihujiwa na uongozi wa Toto African.
Wakizungumza mjini hapa juzi, baadhi ya wachezaji hao (majina yanahifadhiwa) walidai kuwa, uongozi wa Toto African hauitakii mema timu yao na unafanya juhudi za makusudi za kuihujumu.
“Kinachofanyika ni kwamba Toto African imekuwa ikifanya mikakati ya makusudi ya kuzisaidia timu zingine tunazocheza nazo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ili tufungwe,”alisema mmoja wa wachezaji hao.
Mchezaji huyo alisema, hujuma hizo pia zilifanyika katika mechi kati yao na Ruvu Shooting, iliyochezwa wiki mbili zilizopita kwenye uwanja huo, lakini hazikufanikiwa. Simba iliichapa Ruvu Shooting mabao 2-1.
Mchezaji mwingine aliongeza kuwa, siku zote Toto African haiitakii mema Simba kutokana na kuwafanyia hujuma kila wanapocheza kwenye uwanja huo, lakini sasa wamezibaini na watapigana kufa na kupona kuishinda.
Aliongeza kuwa, kinachofanywa na Toto African ni kuhakikisha Simba inafungwa mechi zake zote za Mwanza ili wahame katika mji huo na kuhamishia kituo chao kwingine.
Simba inatarajiwa kupambana na Toto African keshokutwa katika mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Mabingwa hao watetezi wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, wakiwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi nne, nyuma ya wapinzani wao wa jadi Yanga, wanaoongoza kwa kuwa na pointi kumi.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri alisema, wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa, wanashinda mechi zao zote zilizosalia.
Phiri alisema kuanzia mechi yao ya keshokutwa dhidi ya Toto African, amepanga kuwatumia baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi, akiwemo kipa namba moja Juma Kaseja.
Kaseja hakuweza kuichezea Simba tangu ligi hiyo ilipoanza, kufuatia kuvunjika kidole cha mkono wakati wa mazoezi ya timu ya taifa, Taifa Stars. Tayari kipa huyo ameshaanza mazoezi na wenzake.
Kocha huyo amewatupia lawama wachezaji wake kwa kucheza chini ya kiwango, hasa safu ya ushambuliaji, ambayo alisema imekuwa ikipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga mabao.
Naye Kocha Mkuu wa Toto African, Choki Abeid alisema Simba isitafute mchawi, aliyesabisha wafungwe na Polisi kwa sababu kiwango chao msimu huu kimeshuka.
Alisema kikosi chake kimejiandaa vyema kukabiliana na Simba na kuongeza kuwa, watahakikisha wanatoka uwanjani na pointi zote tatu.

No comments:

Post a Comment