KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 2, 2010

Sikinde kula Idd el Fitri mikoani

BAADA ya mapumziko ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ imepanga kula sikukuu ya Idd el Fitr katika mikoa ya Mara, Geita na Kagera.
Msemaji wa bendi hiyo, Emmanuel Ndege alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wamealikwa kufanya maonyesho katika miji hiyo na Kampuni ya JOFAT Entertainment ya Mara.
Ndege alisema bendi hiyo itafanya onyesho lake la kwanza siku ya Idd Mosi kwenye ukumbi wa Bwalo la Magereza mjini Musoma na kufanya onyesho la pili siku ya Idd Pili kwenye ukumbi wa Ambassador Pub wa mjini Geita.
Alisema onyesho la tatu litafanyika Idd Tatu kwenye ukumbi wa New Kahama uliopo mjini Kahama kabla ya kuhamishia mashambulizi yao mjini Biharamulo Septemba 16 mwaka huu.
Ndege alisema maonyesho mengine yatafanyika Septemba 17 mwaka huu kwenye ukumbi wa California mjini Muleba kabla ya kuhitimisha ziara yao Septemba 18 kwa kufanya onyesho kwenye ukumbi wa Lines mjini Bukoba.
Msemaji huyo amewashukuru Mkurugenzi wa JOFAT, Fatuma Mavazi na meneja wake, Joseph Mbwiliza kwa kufanikisha ziara hiyo, ambayo alisema wanatarajia itakuwa ya aina yake.
Alisema wamepanga kuitumia ziara hiyo kuwaonyesha mashabiki wa miji hiyo makali ya bendi yao kimuziki na pia kutambulisha nyimbo zao kadhaa mpya.
Amewataka mashabiki wa miji hiyo kukaa mkao wa kula kwa vile watapata burudani safi na murua, ambayo huenda hawajaipata katika kipindi kirefu cha maisha yao.
Amewaomba radhi mashabiki wao wa mjini Dar es Salaam kwa kutokuwa nao wakati wa sikukuu hiyo na kuwataka wajiandae kupata burudani kabambe baada ya bendi hiyo kurejea maskani yake DDC Kariakoo.

No comments:

Post a Comment