'
Wednesday, September 22, 2010
TENGA: CECAFA imepata mafanikio makubwa
RAIS wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga amekiri kuwa, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya soka katika nchi za ukanda huu wa Afrika ikilinganishwa na miaka iliyopita. Tenga alisema hayo alipohojiwa na mtandao wa Cafonline hivi karibuni. Makala hii ya Cafonline inafafanua zaidi.
Cafonline: Kipi unachoweza kusema kuhusu maendeleo yaliyoletwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA)?
Tenga: Tumeleta maendeleo makubwa, hasa katika kuwavutia wadhamini zaidi katika michuano yetu na kuleta ushindani zaidi kwa sababu viwango vya zawadi vimeongezeka katika michuano ya Kombe la Chalenji na Kombe la Kagame. Pia kuzialika timu kama Zambia na Malawi katika Kombe la Chalenji kumesaidia kuwapa nafasi ya kujifunza wachezaji wa ukanda wetu.
Cafonline: Kwa nini nchi za ukanda wa CECAFA zimekuwa zikipata tabu kufuzu katika fainali za Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika?
Tenga: Kadri tulivyoweza kuleta maendeleo katika ukanda huu, nafikiri hatukuwekeza vya kutosha katika masuala yanayohusu soka ya vijana kama walivyofanya kaka zetu wa Kaskazini, Kusini na Magharibi mwa Afrika wanavyofanya mipango kwa ajili ya Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika. Soka ni biashara kubwa na tunahitaji kuwekeza zaidi katika kuwapa mafunzo makocha na pia masuala ya utawala kama tunataka kufuzu kucheza michuano mikubwa ya Kombe la Dunia na pia siku zote kuwa na timu katika fainali za Mataifa ya Afrika.
Cafonline: CECAFA inadhani kwamba kuzileta timu mwalika katika michuano yake kunaweza kuleta miujiza?
Tenga: Katika njia moja au nyingine, ni kweli tunapata mafanikio kwa kuzialika timu hizi. Siku zote nimekuwa nikimshukuru Rais wa Chama cha Soka cha Zambia, Kalusha bwalya, ambaye siku zote amekuwa akituma timu tunapowaalika. Ndani ya shirikisho letu, pia tunafikiri mambo makubwa zaidi na hii itasaidia kuleta maendeleo ya muda mrefu katika ukanda wetu. Kwa mfano, Uganda inaanzisha ligi ya kulipwa mwaka huu na sisi Tanzania tutafuata nyayo hizo msimu ujao.
Cafoline: Ni vipi CECAFA na mashirikisho yake katika ukanda huu yanavyoweza kumudu kuwa na udhamini katika kipindi hiki kigumu wakati baadhi ya kampuni zimekuwa zikijitoa katika kudhamini soka?
Tenga: Japokuwa serikali katika nchi zinazounda CECAFA zinachukua nafasi kubwa katika kudhamini soka, kampuni binafsi zimekuwa zikijitokeza kuunga mkono mchezo huo. Kwa mfano, nchini Uganda wiki iliyopita, Kampuni ya MTN imetoa dola 700,000 za Marekani kwa ajili ya maendeleo ya timu ya taifa na soka ya vijana. Katika nchi kama Tanzania, Rwanda na Kenya, ligi zinadhaminiwa na kampuni binafsi na haya ni mafanikio makubwa.
Cafonline: Katika michuano ya hivi karibuni ya vijana wa chini ya miaka 20 iliyofanyika Eritrea, kulikuwepo na malalamiko ya kudanganya umri wa wachezaji kwa baadhi ya timu na Zanzibar ilitolewa kwa sababu ya kosa hilo. Unasemaje kuhusu hili?
Tenga: Udanganyifu wa umri ni tatizo kubwa si kwa sababu michezo ni amani na unapaswa kufuata sheria. Lakini tatizo hilo halipo katika nchi za ukanda wetu pekee, lipo zaidi Afrika Magharibi na Asia. Katika CECAFA tumechukua hatua madhubuti kuhakikisha tunakabiliana nalo, japokuwa tunapaswa kuendelea kuwaelimisha watu kuhusu hilo. Tutaendelea kuwa makini na wakali katika jambo hilo na kuchukua hatua kali kwa wahusika.
Cafonline: Unadhani kuwa na wanasoka wengi wa kulipwa ni muhimu kwa timu ya taifa, hasa katika ukanda wenu ili kuzisaidia nchi kufuzu kucheza katika michuano mikubwa?
Tenga: Binafsi, naamini tunapaswa kuwapa nafasi wachezaji wote kwenda kucheza soka ya kulipwa nje bila kuwazuia kwa sababu kutafungua milango zaidi kwa maendeleo ya soka katika siku zijazo. Tazama nchi za Afrika Magharibu kama Nigeria yenye wanasoka wengi wa kulipwa. Kumewasaidia kupata soko la wachezaji wengi zaidi na pia timu yao ya taifa tangu wachezaji hao walipoanza kwenda nje na kufanya kila kitu kitaalamu na pia kuwa na nidhamu. Acha tupeleke wanasoka wengi kadri iwezekanavyo kucheza soka ya kulipwa na matunda yake utayaona.
Cafonline: Una maoni gani kuhusu ushiriki wa timu za CECAFA katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za 2012?
Tenga: Nafikiri karibu timu zote zilizocheza nyumbani, zilishinda mechi zake ukiondoa Ethiopia na huu ni mwanzo mzuri. Kwa timu kufuzu katika michuano hiyo, siku zote ni muhimu kupata pointi zote za nyumbani na pia kupata pointi chache ugenini. Nilipata furaha kubwa niliposikia kwamba nchi yangu Tanzania ilipata pointi moja ugenini dhidi ya Algeria. Lakini timu zote za ukanda wa CECAFA hazipaswi kubweteka, zinapaswa kuendelea kuwa makini katika michezo yote.
Cafnline: Michuano ya vijana wa chini ya miaka 20 iliyofanyika Eritrea ilikuwa na mafanikio gani? Na Tanzania inajiandaaje kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika Novemba hadi Desemba mwaka huu?
Tenga: Michuano ya Eritrea ilikuwa na ushindani mkubwa na ilitusaidia kuvumbua vipaji vipya vya vijana. Kujumuishwa kwa Yemen kama timu mwalikwa pia kulitusaidia kwa sababu kuliwapa nafasi ya kujifunza wachezaji wetu vijana. Lakini mwisho wa mashindano, timu bora, Eritrea na Uganda zilifuzu kucheza fainali na mabingwa watetezi Uganda walitwaa ubingwa kwa njia ya penalti.
Kama CECAFA, tunafanya kila tunaloweza kuona kwamba tunakuwa na michuano mizuri ya Kombe la Chalenji nchini Tanzania na tayari chama cha soka cha Tanzania kimeanza kutafuta wadhamini kwa lengo la kuifanya iwe na mafanikio makubwa zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment