KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 16, 2010

SIMBA YAPETA, YANGA YABANWA



MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Vodacom, Simba jana waliendelea kuvuna pointi tatu baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ ndiye aliyeibeba Simba baada ya kuifungia mabao yote mawili, dakika ya tano na 20 wakati bao la kujifariji la Ruvu Shooting lilifungwa na Mashaka Maliwa dakika ya 16.
Kwa matokeo hayo, Simba bado inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi tisa baada ya kucheza mechi tatu na kushinda zote wakati Ruvu Shooting haina pointi hadi sasa.
Wakati huo huo, timu kongwe ya Yanga jana ilibanwa mbavu baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Sare hiyo iliifanya Yanga iendelee kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi saba baada ya kucheza mechi tatu wakati Mtibwa ni ya tano kwa kuwa na pointi tano baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Pambano hilo lilianza kwa kasi huku kila timu ikipania kuwa ya kwanza kupata bao. Yanga nusura ipate bao dakika ya sita wakati Jerry Tegete alipopewa pasi akiwa nje kidogo ya mita 18, lakini shuti lake lilitoka nje.
Mtibwa ilifanya shambulizi kali kwenye lango la Yanga dakika ya 23 wakati Yona Ndabila alipoingia na mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Yaw Berko.
Dakika mbili baadae, kibao kiliigeukia Mtibwa baada ya Nsa Job kupewa pasi safi akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Shabani Kado.
Mtibwa ilihesabu bao lake dakika ya 33 kupitia kwa Obadia Mungusa, aliyeunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Yusuf Ndula.
Yanga ilisawazisha dakika ya 73 kwa bao lililofungwa na Abdi Kassim kwa shuti la umbali wa mita 30 lililotinga moja kwa moja wavuni.

YANGA: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Isaack Boakye, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Ernest Boakye, Athumani Iddi ‘Chuji’, Abdi Kassim/Nurdin Bakari, Jerry Tegete/Yahya Tumbo, Nsa Job na Geofrey Bonny.
MTIBWA:Shabani Kado, Juma Abdul, Yusuf Nguya, Obadia Mungusa, Salvatory Ntebe, Shaaban Nditi, Zuberi Katwila, Masoud Chile/Ally Mohamed, Thomas Maurice/Saidi Rashid, Yona Ndabila, Salum Machaku.

No comments:

Post a Comment