KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 22, 2010

KARUME, MAALIM SEIF KUSHUHUDIA MECHI YA SOKA

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad wanatarajiwa kushuhudia mechi ya soka ya kirafiki kati ya timu za kombaini za Unguja na Pemba .
Mechi hiyo itakayochezwa Oktoba Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan, imeandaliwa na Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kwa lengo la kuunga mkono maridhiano yaliyofikiwa na viongozi hao wawili na kuridhiwa na wananchi wote wa Zanzibar .
Mbali na viongozi hao wawili, ZFA pia imetoa mwaliko kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM na mgombea mwenza wa urais wa Tanzania , Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai alisema mjini hapa juzi kuwa, tayari chama chake kimeshatuma mwaliko kwa viongozi hao kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo ya kihistoria.
Attai alisema kutokana na umuhimu wa pambano hilo , wana hakika viongozi hao wataungana na mashabiki wa soka wa Zanzibar kuwashuhudia vijana kutoka visiwa hivyo viwili wakisakata kabumbu.
Aliongeza kuwa, mipango inafanywa ili Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna awe mgeni rasmi katika mechi hiyo.
“Tayari vikosi vya timu hizo mbili za Unguja na Pemba vimeshapatikana na vimeshaanza maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo, inayolenga kuwaunga mkono viongozi wetu katika kufikia maridhiano kwa ajili ya kuijenga upya Zanzibar ,”alisema.
Kwa mujibu wa Attai. Kocha Mkuu wa Zanzibar , Stewart John Hall atautumia mchezo huo kuteua wachezaji watakaounda kikosi cha timu ya visiwa hivyo, itakayoshiriki katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji itakayofanyika Novemba mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, fedha zitakazopatikana katika mechi hiyo, zitatumika kuchangia maandalizi ya Zanzibar katika michuano ya Chalenji, itakayozishirikisha timu za mataifa yanayounda ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

No comments:

Post a Comment