KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 2, 2010

NSAJIGWA: Tutawafunga Waalgeria kwao


SWALI: Ukiwa nahodha wa Taifa Stars, mnakwenda kucheza na Algeria, ukiwa ni mchezo wa kwanza wa michuano hiyo chini ya kocha mpya, Jan Poulsen. Nini matarajio yenu katika mechi hiyo?
JIBU: Ni kweli kuna mabadiliko kidogo katika timu yetu, lakini makocha wote wawili ni wazuri, wamekuwa wakitufundisha mbinu za hali ya juu na kila mchezaji ana hamu kubwa ya kutaka kuifunga Algeria kwao ili tujiweke kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kocha Poulsen ameonyesha uwezo mkubwa wa kufundisha soka kama ilivyokuwa kwa Marcio Maximo, ambaye kwa kweli tunamshukuru kwa kazi kubwa aliyofanya, licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo, ambazo ni za kawaida kwa binadamu yoyote.Kwa kifupi ni kwamba kikosi chetu kimejiandaa vyema kwa pambano hilo.
SWALI: Tumeona mara baada ya Poulsen kuanza kuifundisha Taifa Stars, aliwaita wachezaji, Athumani Iddi na Juma Kaseja, ambao Maximo aliwatema kwenye kikosi chake. Una maoni gani kuhusu kitendo hicho cha Poulsen?
JIBU: Kwa kawaida, kila kocha ana mawazo na mtazamo wake. Ninachoweza kusema ni kwamba huo ni uamuzi wake, ambao amejipangia kwa lengo la kutimiza majukumu yake. Isipokuwa napenda kusema kuwa hayo ni mambo mazuri, ambayo yamelenga kuiletea mafanikio mazuri timu yetu.
SWALI: Hivi ni kweli mmejidhatiti vyema kuishinda Algeria kwao ama ni maneno ya kujipa moyo tu? Mliwaona walivyocheza kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka huu Afrika Kusini?
JIBU:Tumeona na kujifunza mengi kuhusu Algeria. Ni timu nzuri na ngumu, lakini na sisi tumejipanga vizuri kukabiliana nao nyumbani kwao. Tumefanya mazoezi ya nguvu kuhakikisha kwamba tunakwenda kushinda.
Pia tumejifunza mbinu zao zote za kimchezo, ndani na nje ya uwanja. Tumeshaujua mfumo wanaoutumia wanapocheza nyumbani kwao na hata ugenini. Hatuoni sababu, ambazo zitatufanya tufungwe katika mchezo huo kama tutayafuata vyema maelekezo ya kocha wetu. Hata hivyo, tutalazimika kucheza kwa tahadhari kubwa.
SWALI: Kipi hasa kinachowapa moyo na nguvu ya kujigamba kwamba mnao uwezo wa kuifunga Algeria nyumbani kwao?
JIBU: Siku zote mchezo wa mpira wa miguu ni maandalizi. Tunazo sababu tatu za msingi za kuishinda Algeria kwao. Ya kwanza tunakwenda kushindana baada ya kufanya maandalizi ya kutosha, pili kikosi chetu kimekamilika katika kila idara na ya tatu wachezaji wote tumekuwa tukipatiwa huduma zote muhimu, kwa maana hiyo hatuna kisingizio tukifungwa.
SWALI: Una maoni gani kuhusu wadhamini wa Taifa Stars, ambao wamekuwa wakijitolea kuisaidia timu yenu kwa kuipeleka nje ya nchi kufanya mazoezi kabla ya kushiriki michuano mikubwa?
JIBU: Hilo ni jambo muhimu katika soka. Kwa upande wetu sisi wachezaji, hatuna cha kusema zaidi ya kucheza soka ya ushindani ili kuwaongezea nguvu ya kutudhamini zaidi. Lakini ukweli ni kwamba, mnapokwenda kufanya mazoezi nje ya nchi, mnajenga uwezo wa kujiamini zaidi na pia kuwa tayari kukabiliana na lolote.
Tunawashukuru sana wadhamini wetu, Kampuni ya Bia ya Serengeti na Benki ya NMB na wadhamini wengine, ambao wamekuwa wakijitolea kutusaidia kwa hali na mali. Pia hatutakuwa na shukurani iwapo hatutamtaja Rais Jakaya Kikwete, ambaye kwa kiasi kikubwa ameleta changamoto ya aina yake katika mchezo wa soka.
Vilevile kwa niaba ya wachezaji wenzangu, tunapenda sana kumshukuru Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kufanikisha ujenzi wa uwanja mpya wa soka, ambao umeiwezesha Taifa Stars kupata nafasi ya kucheza na timu kubwa duniani kama vile Brazil, Cameroon, Ivory Coast na zinginezo na kukutana na baadhi ya wachezaji nyota duniani, ambao hatukuwa na mawazo iwapo siku moja tutacheza nao ana kwa ana.
SWALI: Ndani ya kikosi chenu kuna baadhi ya wachezaji, ambao wanacheza nje ya nchi na wengine wanacheza hapa nyumbani. Kuna tofauti yoyote kati yenu, ambayo umeshaiona hadi sasa?
JIBU: Tofauti ipo, tena kubwa tu, lakini bado kuna wachezaji wengi wazuri hapa nyumbani, lakini hawajapata bahati ya kupata timu nje. Kinachotakiwa kufanyika ni wachezaji hawa kuongeza bidii katika mazoezi ili uwezo wao uweze kuongezeka.
Yapo mafanikio mengi kisoka na kimaisha yaliyopatikana kwa wanasoka wa Tanzania waliopo nje ya nchi. Na hii ni changamoto kubwa kwetu sisi tuliopo hapa nyumbani kuongeza juhudi ili tuweze kupata nafasi hiyo.
SWALI: Tumeona kuna matatizo kwa baadhi ya wachezaji, ambao wanakwenda kufanya majaribio ya kucheza mpira wa kulipwa nje ya nchi, ambapo huwalalamikia mawakala kwa kutokuwa wakweli. Una maoni gani kuhusu jambo hilo?
JIBU: Sina hakika sana kuhusu malalamiko, ambayo yamekuwa yakitolewa na wachezaji kwa mawakala hao. Lakini kama kuna mawakala au viongozi wanaotaka kufanya ujanja wa kuwanyima haki wanazostahili wachezaji, hili jambo si sahihi na linapaswa kupigwa vita kwa sababu kila mtu anafanyakazi ili apate kula.
SWALI: Una maoni gani kuhusu utaratibu mzuri wa kuwapata wachezaji wa Taifa Stars, ili timu hiyo iweze kutisha zaidi katika mashindano ya kimataifa?
JIBU: Mimi binafsi nafikiri kuna umuhimu zaidi wa kumpa nafasi Kocha Paoulsen aweze kupanga mikakati yake ya kutafuta wachezaji ili aweze kuwa na kikosi imara na kitakacholeta heshima kwa nchi kimataifa.
SWALI: Una ushauri gani kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu kuziimarisha timu za Taifa Stars, Ngorongoro Heroes, Serengeti Boys na Twiga Stars?
JIBU: Wanapaswa kuzitafutia wadhamini timu zote nne, yaani kila moja iwe na mdhamini wake. Hii itasaidia kuongeza hamasa zaidi kwa wachezaji, kuliko ilivyo hivi sasa, ambapo udhamini mkubwa upo kwa Taifa Stars na kuziacha timu zingine zikisuasua katika ufadhili.
Hali hii imesababisha TFF iwe na wakati mgumu katika kuziandaa timu zingine tatu zinaposhiriki michuano ya kimataifa. Nawaomba wafanyabiashara na kampuni mbalimbali zijitokeze kuzidhamini timu hizo tatu ili nazo ziweze kufika mbali na kupata mafanikio makubwa zaidi kisoka.

No comments:

Post a Comment